Twiga Stars, Ghana kundi moja

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:24 AM Nov 24 2024
TIMU ya Soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars)
Picha: Mtandao
TIMU ya Soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars)

TIMU ya Soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), imepangwa Kundi C pamoja na mabingwa watetezi, Afrika Kusini (Banyana Banyana), Ghana na Mali katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (WAFCON).

Fainali za WAFCON zitafanyika kuanzia Julai 5 hadi 26, mwakani nchini Morocco.

Katika droo iliyofanyika jijini Rabat juzi, wenyeji Morocco wamepangwa katika Kundi A pamoja na Zambia, Senegal na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo).

Droo hiyo iliyofanyika mbele ya Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dk. Patrice Motsepe, ilishuhudiwa mabingwa mara nyingi, Nigeria wakiangukia Kundi B pamoja na Algeria, Tunisia na Botswana.

Mara ya kwanza Twiga Stars kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake ilikuwa mwaka 2010 na iliishia hatua ya makundi.

Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Tanzania (TWFA), Somoe Ng'itu, aliliambia gazeti hili hakuna kundi rahisi katika fainali hizo.

Alisema maandalizi kuelekea fainali hizo yameshaanza ambapo mwezi uliopita Twiga Stars ilisafiri kwenda Morocco kucheza michezo miwili ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya wenyeji na Senegal.

"Hakuna kundi rahisi, timu zote 12 zilizofika hatua hiyo ni bora, tumejipanga kwenda katika fainali hizo kama washindani, tunaamini tutapeperusha vyema bendera ya Tanzania," alisema Somoe.