MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Ndomba, amesema kuanzishwa kwa mamlaka hiyo, kumeiwezesha serikali kudhibiti moja kwa moja, mifumo na miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), serikalini sambamba na kuilinda.
Ndomba, ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mkutano wa tano wa Serikali Mtandao unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo umebebwa na kauli mbiu isemayo, ‘Jitihada na ubunifu wa serikali mtandao kwa utoaji huduma za umma kwa ufanisi’.
Anasema mamlaka imeweza kukabiliana na viashiria na matishio ya kiusalama mtandaoni, kwa taasisi za umma kwa kiwango kikubwa, kutokana na kuwatumia wataalamu wa ndani waliojengewa uwezo katika eneo hilo.
Anasema wataalamu hao wamewezeshwa kutatua matatizo mengi, kupitia mifumo yao waliyoisadifu, kuijenga na kuiendesha ambayo hutumika kwa taasisi za umma.
“Katika kukabiliana na matukio ya usalama wa mtandaoni, mamlaka hutoa msaada wa kimifumo na ushauri kuhusu usalama wa TEHAMA, viashiria na matishio ya kiusalama mtandaoni kwa taasisi za umma na kukabiliana na mashambulio ya kimtandao yanapotokea,” anasema.
Ndomba anasema yote hayo hufanyika kwa kutumia wataalamu wa ndani.
Aidha, anasema katika kuhakikisha mifumo na miradi ya TEHAMA inaleta tija iliyokusudiwa, mamlaka huandaa viwango na miongozo ya Serikali Mtandao ambayo taasisi za umma hutakiwa kuifuata wakati wote.
Anasema katika jitihada ya kuendana na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea duniani, mwaka 2019 mamlaka ilianzisha Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Serikali Mtandao, ambacho hutumika kufanya utafiti na kutatua changamoto zilizoko nchini, ili kuboresha utendaji kazi serikalini.
Ndomba anasema kituo hicho hufuatilia matumizi ya teknolojia zinazoibukia na kuangalia zinazoweza kutumika na kuleta matokeo chanya.
Pia anasema, ili kufikia hayo, mamlaka imeingia makubaliano na taasisi za elimu ya juu na zile za utafiti kikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Sayansi na Teknolojia na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Anasema baadhi ya mifumo iliyojengwa kupitia kituo hicho ni pamoja na ule wa e-Mrejesho ambao ulitambuliwa na kupewa tuzo mwezi Septemba, 2024 na Umoja wa Mataifa, kama mfumo bora unaounganisha serikali na wananchi kidigiti kwa kuwezesha kuwasiliana.
Ndomba anasema ushirikiano wa eGA na Wakala wa Serikali Mtandao Zanzibar katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao, si tu umewezesha kujenga uwezo kwa wataalamu hao, pia umewezesha kuiainisha ukuaji Serikali Mtandao katika taasisi za umma pande zote mbili, Bara na Visiwani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala Serikali Mtandao Zanzibar, Saidi Seif Said, amepongeza Mamlaka Serikali Mtandao, kwa jitihada kubwa inazofanya kuboresha sekta ya umma.
Seif anasema mafanikio makubwa yaliyoainishwa kupitia mkutano huo unaoendelea, yamerahisisha utoaji huduma kwa wananchi na kuimarisha utendaji kazi katika serikali hizo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED