TGNP yatoa mafunzo ya usawa wa kijinsia kwa waandishi wa habari

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 03:34 PM Dec 30 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi.

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umetoa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari kutoka mikoa zaidi ya 10 nchini, yakilenga kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya usawa wa kijinsia.

Mafunzo hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki katika ofisi za TGNP jijini Dar es Salaam katika kuelekea kumbukizi ya miaka 30 ya Mkutano wa Beijing, uliofanyika mwaka 1995.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, alisema kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhamasisha jamii kuelewa na kuzingatia usawa wa kijinsia.

"Lengo letu ni kuhakikisha waandishi wa habari wanapata maarifa ya kina ya kuandika na kuripoti habari zinazogusa masuala ya kijinsia kwa usahihi na weledi," alisema Liundi.  

Alisema kuwa jinsia ni agenda ya maendeleo na hivyo ni muhimu kutokuachwa kundi nyuma katika mchakato wa kuleta maendeleo katika nchi yoyote duani.Mafunzo hayo yameongeza ufahamu kwa wanahabari na wamejipanga kutumia vyombo vya habari kuelimisha jamii.  

Alisema TGNP imeweka msisitizo wa kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuwa sehemu muhimu ya ajenda za kitaifa, huku ikihimiza ushirikiano wa vyombo vya habari katika kufanikisha malengo hayo.

Mkutano wa Beijing, uliofanyika mwaka 1995, ulikuwa wa kihistoria kwa kuwa uliwakutanisha wanawake kutoka mataifa mbalimbali duniani kujadili masuala ya usawa wa kijinsia, haki za binadamu, na maendeleo ya wanawake.

Mkutano huo ulibeba maazimio yaliyolenga kuimarisha nafasi ya wanawake katika jamii na kupunguza pengo la kijinsia, ambayo bado yanahitajika kufanyiwa kazi kwa kina.