UCHAGUZI WA MWENYEKITI... Lema atoa hadhari CHADEMA kufa

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:03 AM Dec 30 2024
Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.

WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikiwa katika maandalizi ya uchaguzi wa viongozi wake ngazi ya taifa, Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amewaonya wanachama na wafuasi wa chama hicho dhidi ya minyukano inayoendelea.

Amesema wanachopaswa kufanya hivi sasa ni kurudi kwenye malengo yao, huku akisisitiza kuwa wakipoteza mwelekeo wa kusudi lao, kuna hatari na chama chao kufa.

Alitoa tahadhari hiyo juzi kupitia ukurasa wake wa X (zamani twiter), akisema vita inayoendelea hivi sasa ndani ya wanachama wenyewe kwa wenyewe ni kubwa na ni hatari kwa mustakabali wa chama.

Lema ambaye ni Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, alisema kwa hali ilivyo, wanachama wa chama hicho wao kwa wao wanapigana vita vikali kutokana na mgawanyo uliotokana na viongozi wanaowaunga mkono ambao wanagombea nafasi za juu za uongozi kitaifa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

"Kwa hali ilivyo sasa, tuna uchungu sisi kwa sisi kuliko tulivyo na uchungu dhidi ya CCM (Chama Cha Mapinduzi).

"Kampeni ya sasa ya dhihaka na matusi kwa viongozi na wananchi ambao hatuwaungi mkono imekuwa kali kuliko kampeni ya kukomesha mauaji na utekaji nchini," "Let’s get back to the purpose (turudi katika kusudio) na kila mtu aheshimiwe na kuthaminiwa kwa upande aliochagua kwa maana ndiyo demokrasia," Lema alisema.

Pia aliwatahadharisha wanachama na wafuasi wa chama hicho kwamba ni vyema wakatambua kwamba mnyukano wa wao kwa wao unaoendelea mitandaoni, unafuatiliwa na wapinzani wao na watautumia katika kampeni za uchaguzi mkuu mwakani.

Alisema hatari nyingine kubwa kwa chama hicho ni kwamba hata wananchi wanawafuatilia kwa karibu na kusambaza kila habari inayoleta fitina ndani ya chama hicho.

"CCM wanatufuatilia sana, wanahifadhi kila kauli zetu juu ya wagombea wetu wote katika mchakato wa uchaguzi wa viongozi wakuu Januari. Bila shaka watazitumia kauli hizi mwaka 2025 kama tutashiriki na kama kutakuwapo na uchaguzi huru," Lema alionya.

Kada huyo wa CHADEMA alisema wananchi wanatumiana kila habari inayoleta fitina na uchungu miongoni mwao, akihadharisha kuwa "hii ni hatari!". 

Alisema chama cha siasa za upinzani ni harakati za kutafuta utawala bora zinazoongozwa na kile alichokiita "kusudio la ndani na moyo wa kujitoa".

"Kusudi likifa, chama kinakufa kwa sababu asilimia 99 ya viongozi na wanachama wanafanya wajibu wa kazi za chama kwa kujitolea. Sasa watawezaje kujitolea kama hakuna purpose (kusudi)? Ari inajengwa na nidhamu," alifafanua.

Tangu kutangazwa kuanza kwa mchakato wa kuchukua fomu za kuwania nafasi za uongozi ndani ya CHADEMA, mpaka sasa waliochukua fomu ya kuwania nafasi ya uenyekiti ni Freeman Mbowe, Tundu Lissu, Romanus Mapunda na Charles Odero.

Mnyukano umekikumba chama hicho baada ya viongozi wakuu wa chama hicho, Mwenyekiti Mbowe na Makamu wake Lissu kutangaza kuchuana katika nafasi ya juu kabisa ya chama chao.

Baadhi ya wanachama wanamuunga mkono Mbowe, wakitaka aendelee kwenye nafasi hiyo kwa awamu nyingine. Kuna kundi lingine linamuunga mkono Lissu, likiamini ni wakati wa kupata kiongozi mpya wa kuongoza chama hicho.