UTAFITI uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) umebaini ongezeko kubwa la matumizi ya viuatilifu katika kuzalisha mboga za majani, hata kuchangia ongezeko la magonjwa hatari nchini.
MUHAS wamebaini ongezeko hilo limepiku matumizi ya viuatilifu katika kilimo cha pamba na kahawa ambacho kwa muda mrefu kilitumia zaidi kemikali hizo.
Matokeo ya utafiti huo uliofanywa katika mikoa yote nchini, yanaonesha matumizi ya viuatilifu kwenye uzalishaji mboga za majani yanachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa kwa binadamu kama vile saratani, kisukari na matatizo ya uzazi.
Mhadhiri na Mtafiti Mwandamizi wa MUHAS, Dk. Vera Ngowi, wakati wa kongamano la kujadili viuatilifu vya kuulia wadudu na afya nchini na Afrika Mashariki lililofanyika MUHAS, alisema matumizi ya viuatilifu kwenye kilimo cha mboga za majani yanahatarisha afya za wananchi.
Alishauri kuongeza kampeni ya kutoa elimu na uhamasishaji kuhusu hatari za matumizi ya viuatilifu kwa afya ya binadamu.
Alisema mamlaka pia zinapaswa kuweka kipaumbele kwa utekelezaji thabiti wa kanuni za viuatilifu ili kuondoa vilivyopigwa marufuku na kuongeza ufuatiliaji wa kanuni.
"Miaka ya nyuma kulikuwa na matumizi makubwa ya viuatilifu kwenye mazao ya pamba na kahawa. Hali imebadiika, uzalishaji wa mboga za majani hivi sasa unatumia kiwango kikubwa, jitihada zinahitajika kukabiliana na suala hilo ili kunusuru afya za wananchi," alisema Dk. Ngowi.
Aliwashauri wakulima kutumia mbinu mbadala zisizo na kemikali za kudhibiti visumbufu kama vile usimamizi ili kupunguza utegemezi wa kemikali zenye kemikali hatari za viwandani pamoja na kuongeza ushirikiano baina ya wakulima, watumiaji na mashirika ya kijamii ili kuongeza uelewa na kukuza kampeni za msingi za mabadiliko ya sheria za usimamizi wa viuatilifu.
"Pia tuna jukumu la kutoa motisha kwa wakulima kufanya kilimo hai na mbinu nyingine zinazopunguza athari kama vile viuatilifu vya kibaiolojia," alisema.
Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema waliamua kufanya utafiti wa athari za viuatilifu kwa afya ya wananchi kwa kuwa hilo ni eneo ambalo halijafanyiwa utafiti kulinganisha na mengine.
Alisema utafiti huo ambao wameufanya kwa ushirikiano na wataalamu wa Norway, kikiwamo Chuo Kikuu cha Oslo na Ubalozi wa Ufaransa nchini, unalenga kuangalia athari za kiafya kwa binadamu kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu na mabadiliko ya tabianchi.
"Tunaangalia maeneo ambayo yanaathiri afya ya binadamu, yakiwamo matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu. Baada ya kongamano hili, tutengeneze mapendekezo kama vile sera au aina gani ya elimu itolewe kwa makundi mbalimbali ya watu.
"Utafiti huu pia unalenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanasababisha vitu mbalimbali kubadilika, hata matumizi ya viuatilifu, aina za wadudu, magonjwa ya binadamu na mazao, hivyo tunaangalia ni kwa namna gani viuatilifu vitatumiwa kwa usahihi," alisema Prof. Kamuhabwa.
Joseph Bilago, Mkuu wa Afya Kazini, aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu, alisema kongamano hilo linalohusu matumizi ya viuatilifu kwenye shughuli za kilimo, afya na mifugo, litasaidia kuona namna matumizi hayo yanakuwa bora katika kulinda afya ya jamii na kupata mazao yanayozingatia matumizi sahihi ya viuatilifu hivyo.
"Viuatilifu vinatumika kwenye kilimo na kukabiliana na magonjwa kama vile malaria, vinatumika kuua viluilui vya mbu, hivyo kuna faida za matumizi hayo lakini kuna hasara pia endapo havitatumika ipasavyo hasa katika uzalishaji mboga na matunda kama nyanya, vitunguu, mboga za majani na kukuza mifugo," alisema Bilago.
Aliongeza kuwa matumizi ya viuatilifu hayakwepeki, hivyo ni vyema wananchi wakazingatia matumizi bora ya viuatilifu ili kulinda afya za wananchi, mimea, wanyama na mabadiliko ya tabianchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED