Wazee wataka kuwa na uwakilishi bungeni

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 12:36 PM Feb 19 2025
Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo akiwa na baadhi ya wazee.

BARAZA la Wazee mkoani Arusha limetaka ushirikishwaji katika vikao mbalimbali vya kijamii na ngazi za kimaamuzi ikiwemo bungeni ili kutumia hekima na busara zao kwenye hatua za maamuzi katika kushauri masuala yenye kuleta maendeleo kitaifa.

Baraza hilo limemuomba Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo kupeleka pendekezo hilo kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili ateuwe uwakilishi wa Baraza la Wazee ndani ya bunge.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Arusha Mzee Mhina Mbelwa wakati akizungumza kwenye hafla ya uhamasishaji wa kutoa elimu ya nishati safi kwa viongozi wa baraza hilo.

"Hatuna uwakilishi maeneo mbalimbali ikiwemo bungeni, makundi mengine yote wana uwakilishi lakini kwa bahati mbaya uongozi wa Baraza la Wazee anayeingia pale kama mbunge kutoka kwa wazee hayupo wakati mwongozo unatutaka tupate uwakilishi, katika wale Rais anaowateua basi aangalie na wazee ili tupate uwakilishi," alisema Mbelwa.

Aidha, Mwenyekiti huyo ameiomba Halmashauri ya Jiji la Arusha kutambua uwepo wa Baraza la wazee katika eneo hilo.