‘Goli la Mama’ tamu lakini chungu

By Joseph kulangwa , Nipashe
Published at 05:36 PM Aug 22 2024
Rais Suluhu Hassan.
Picha: Ikulu
Rais Suluhu Hassan.

WANASEMA pesa ni sabuni ya roho. Na wanaosema hivyo ni waliozaliwa katika karne za hivi karibuni, baada ya mapinduzi ya viwanda huko Ulaya! Mapinduzi hayo tumekuwa tukifundishwa kwenye Historia shuleni.

Kwamba bila mabadiliko hayo kufanyika Ughaibuni, bila shaka tungeendelea kuishi kwa kufanya biashara ya kubadilishana mali na si kuuziana kwa sarafu na noti kama ilivyo hivi sasa.

Kama hamkumbuki, basi jueni kuwa zamani tulibadilishana chakula na bidhaa zingine, kama ulikuwa na mtama mimi jembe, ukanipa gunia moja au hata mkuki ulinipa debe la muhogo aka udaga au makopa.

Mapinduzi yakaleta sarafu na noti, na hivi sasa mwenye sarafu au noti ndiye anaheshimika katika jamii. Na kwa ujinga wetu, hata mwenye ng’ombe 100 anaonekana si mali kitu mbele ya mwenye Sh milioni tano!

Fedha tumeipa hadhi kuliko hata hadhi ya binadamu. Unaweza kusikia mtu anasema “nitakupiga nikuue, nikulipe.” Atalipa nini? Fedha! Anadhani thamani ya utu ni sarafu na noti. Mwenye fedha akaitwa tajiri na kufunika mwenye watoto!

Leo mitaani, kuna vijana wanatamba kuwa na fedha, wanaonekana wakizianika kama si kwenye magari bali mifukoni na kwenye mabegi yao na kupita nazo barabarani kuzuga wasionazo.

Tunashuhudia mitandaoni vijana  wakitamba, ukisikia mimi ni kijana mdogo tajiri mwenye fedha na hata kutukana wasionazo kuwa “we mpumbavu unayetazama video hii njoo nikufundishwe jinsi ya kupata fedha!”

Tunashuhudia matajiri mijini wakimiliki mali na hata watu kwa majina ya timu za soka na kupewa vyeo vya wafadhili au wadhamini, kutokana na ukwasi walionao.

Wengine tunawaona kwenye mikusanyiko ya sherehe, hususan harusi wakipita mbele kutuza maharusi, huku wakitapanya fedha sakafuni wakizikanyaga na kushangiliwa na wahudhuriaji kwa kuwaita ‘Tajiri! Tajiri!’, ilimradi wakiwavimbisha vichwa vyana kuzimwaga zaidi.

Juzikati hapa ndugu zangu Mwanza walishuhudia kufuru kama hii, na punde Jeshi la Polisi likawatuliza waliokuwa wakitupa fedha sakafuni na kuwaweka kunakohusika kwa tuhuma za kutoheshimu amana hiyo ya kiuchumi.

Bila shaka wahusika hawajatoa somo la kutosha kuhusu tabia hii ya kurusha na kutupa fedha sakafuni, au kufikicha fedha na kuzificha sehemu za siri kwa baadhi ya watu, lakini pia kuzishika huku mikono ikiwa michafu kama ya ‘Paulo’.

Pengine hatua iliyochukuliwa na dogo Wilbrod Mutafungwa wa Mwanza kwa jamaa zangu wale akina ‘getegete’, litakuwa onyo na funzo kwa wenye nia ya kufanya hivyo, ili kujipatia ujiko kwenye mikusanyiko kama ule.

Lakini pia, pengine hatua kama hiyo inapaswa kuchukuliwa hata kwa wanaojianika na mabulungutu ya noti barabarani au mitandaoni na kutambia wengine, kana kwamba kufanya hivyo kunaongeza tija, au kama si tu kujitangaza kuzipata kwa njia zisizoeleweka.

Serikali inapohimiza watu kuhifadhi fedha zao benki, si kwamba inawahurumia saana wanapokaa nazo majumbani, kuwa labda zinaweza kuibwa au kuungua au kukumbwa na ajali nyingine, ah ah, inataka zizungushwe na kuchangia kwenye uchumi.

Hivyo, kukaa nazo majumbani au kwenye magari ili kuringishia si sawa kabisa, nao wa hivyo hata kama ni wanachama wa ‘Friimasoni’, waelekezwe la kufanya na kuhakikisha ujinga wanaofanya haurudii.

Na ndiyo maana pia, nachukua fursa hii kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuja na ubunifu wa ‘Goli la Mama’ katika michuano ya kimataifa ya klabu za soka za wanaume, ambako amekuwa akinunua kila goli linalofungwa na klabu ya nchini inapocheza na ya ugenini na kushinda.

Lakini natilia shaka jinsi fedha hizo zinavyotolewa, pale ambapo mtoaji hulazimika kusafiri na bulungutu la noti na kukaa nalo uwanjani, sijui kwa usalama upi, na kuja kutoa mwishoni mshindi anapokuwa amepatikana kwa idadi ya magoli fulani yasiyotabiriwa.

Hebu fikiria, kwanza huwa haijulikani mshindi atafunga mangapi. Ina maana fedha huletwa zikiwa hazijui kuwa zitarudi au zitabaki zote. Na ni kiasi gani? Mathalan yakifungwa 10, atakuwa na kiasi gani uwanjani?

Kama makombe huandikwa nani kashinda na kutwaa palepale uwanjani baada ya mechi, kwa nini mleta fedha asije na hundi bandia na kalamu akaandika kiasi cha fedha na mshindi na kukabidhi hundi na fedha kuingizwa kwenye akaunti ya mshindi? Nini kitaharibika? Tujaribu tuone.