Ndivyo kutokurasimisha biashara zao kunavyowaweka kando kimafanikio

By Restuta James , Nipashe
Published at 07:06 AM Aug 23 2024
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bengi’i Issa.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bengi’i Issa.

BIASHARA nyingi hasa za wanawake, hazikidhi baadhi ya matakwa ya kisheria kama kuzisajili, ambayo kama yangezingatiwa, yangewafungulia fursa ya masoko makubwa ya ndani na nje.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa, anasema changamoto inayokabili biashara za wanawake, vijana na wenye ulemavu ni kutorasimishwa, hivyo kukosa fursa ya kupata zabuni.

Anasema sheria ya ununuzi inazitaka mamlaka zote za nchi kuanzia serikali kuu, kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi, kwa ajili ya kampuni za wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.

“Kama tutazipata zikaingia kwenye biashara zetu zitachochea sana ukuaji wa uchumi wenye matokeo makubwa. Nataka niwape hiyo changamato wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na wazee kwamba turasimishe biashara zetu ili tuweze kuteka hizi fursa,” anasema.

Anasema makundi hayo yanapaswa kuzingatia utunzaji wa kumbukumbu za biashara, ubora, kuwa na uwezo wa kutoa huduma baada ya makubaliano na kutumia teknolojia kuingia kwenye mifumo ya kuomba zabuni.

“Zabuni inaweza kukuambia upeleke kiasi fulani kila wiki au mwezi na usiishiwe. Tukiweza kufanikiwa kwenye ubora na uwezo wa kulishika soko, tutaweza kuingia kwenye masoko ya ndani na ya nje,” anasema.

Ili kumudu zabuni kubwa, anashauri kampuni ndogo kuungana kwa lengo la kuzalisha kwa wingi na kwa ubora unaotakiwa. 

Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), kwa kuangalia upungufu huo wa masuala ya kisheria kwenye miradi ya wanawake, kwa kuanzisha programu maalumu ya kuwaelimisha wanawake na vijana namna ya kupata zabuni za umma.

Programu hiyo ‘Bid for success’ ikifupishwa B4S, inataka kuona asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi wa umma inayokadiriwa kuwa zaidi ya Sh. trilioni mbili mwaka huu wa fedha 2024/25, inaingia kwenye kampuni zinazomilikiwa na wanawake pamoja na vijana.

Mwajuma Hamza ni Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, anayeeleza kuwa utafiti wa chemba hiyo wa mwaka 2021, ulibaini kwamba wanawake, vijana na makundi maalumu yanayoshinda zabuni za serikali ni chini ya asilimia mbili.

Anasema utafiti ulifanikisha mabadiliko ya sheria na kutungwa kwa kanuni zinazoelekeza ushiriki wa kila kundi kwenye zabuni za umma ili fedha hizo ziingie kwenye ‘mifuko’ ya makundi hayo maalum.

“Tukasema soko la serikali ni kubwa, bajeti ya mwaka huu wa fedha ni Sh. trilioni 49.3 ambazo asilimia 70 inakwenda kwenye ununuzi. Miradi mikubwa inatekelezwa, sisi wanawake ni lazima tushiriki kwenye fursa hizi, vinginevyo tutakuwa watazamaji,” anasema.

Anasema B4S inalenga kuwapa wanawake na vijana taarifa za masoko na zabuni za umma, namna ya kuomba na kutimiza makubaliano.

“Tunalenga kuwajengea uwezo wanawake na vijana ili wakashindane kwenye zabuni na kuonyesha matokeo. Tunataka kuona ongezeko la wanawake kutumia hii fursa. Kwa mfano, wakati fulani, Wizara ya Ujenzi ilitangaza zabuni ambayo ilitenga Sh. bilioni 80 kwa ajili ya kampuni za wanawake, ni wanawake sita tu ndio waliomba…hii inatupa picha kwamba bado tuna kazi kubwa ya kufanya,” anasema.

“Wakati tunahamasisha na kuhakikisha ofisi za umma zinatenga asilimia 30 kwa ajili ya makundi haya, sisi tuhakikishe wanawake wana uwezo…serikali inaweza kutenga halafu watu wakawa hawana uwezo wa kuzitumia hizi fursa, hatuwezi kwenda mbele,” anasema.

Mkurugenzi Mkazi wa Trade Mark Afrika, Elibariki Shammy, anasema utafiti wa mwaka 2021, ulibaini kwamba baadhi ya watumishi wa Halmashauri na idara za serikali, hawakuwa na uwezo wa kuandaa zabuni inayokidhi uwezo wa kampuni zinazomilikiwa na makundi maalumu.

“Kuna suala la kujenga uwezo na kushirikiana ili zile zabuni zinapoandaliwa, zikidhi mahitaji ya kampuni za makundi haya. Kwenye zabuni ni utaalamu wa kuandika kile kinachohitajika na ushindani wa bei. Walaji wanapochagua bidhaa hawazingatii mzalishaji bali ubora na bei,” anasema.

Anasema: “Masoko siyo shida, tuna hii asilimia 30 ambayo pia hatujaweza kuitumia…bidhaa za Afrika haziuzi sana sokoni kwa sababu ya ubora, bei na uwezo wa kuhudumia soko kwa muda mrefu.”

Anatahadhalirisha kwamba kuomba zabuni ya umma na kushinda ni hatua moja na kulipwa baada ya kutimiza makubaliano ni hatua nyingine.

“Kama tunahitaji kutengeneza uchumi ambao unawalenga wanawake, vijana na makundi maalumu ni muhimu kutazama kwa upana sera na taratibu za biashara ili kuwezesha ukuaji wa uchumi unaowagusa wananchi wengi,” anasema Shammy.

“Serikali inapaswa kuwa na sera madhubuti ya kukuza viwanda vya ndani ili wazawa wanaposhinda zabuni, mzunguko wa fedha ubakie kwenye uchumi nchini. Isipowalipa kwa wakati, kampuni hizi zitakufa mapema na lengo la kuwainua halitafikiwa,” anasema.

Anasema ni muhimu kutengeneza bishara endelevu na hasa viwanda ili kubakisha fedha ndani ya nchi, badala ya kuagiza nje.

“Ili viwanda viwepo ni muhimu sera zizungumze vizuri na mahitaji ya nchi katika maeneo mbalimbali ili kuzalisha ajira na kuondoa umasikini. Hakuna nchi isiyokuwa na utaratibu, lakini usipokuwa rafiki kila mtu anapoteza,” anasema.

Ofisa Mwandamizi katika Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Elias Chaponde, anasema sheria ya PPRA sura na 410 ya mwaka 2023 kifungu cha 64, inazielekeza Halmashauri na ofisi zote za serikali kutenga bajeti yake ya ununuzi kila mwaka kwa ajili ya wazabuni wanawake, vijana na makundi maalumu. 

Anasema kanuni za sheria hiyo (PPR), ambazo zimeanza kutumia mwaka huu wa fedha 2024/2025, zinazitaka ofisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi hayo.

“PPRA kazi yake ni kufuatilia na kusimamia kuhakikisha kwamba taasisi za umma zinatekeleza takwa hilo la kisheria kwa kutenga hiyo asilimia 30 kwa ajili ya wanawake, vijana na makundi maalumu na kutoa ripoti,” anasema.