JARIBU kukumbuka kauli hii ya Oktoba 6, 2016 kutoka Mkuranga, mkoani Pwani: “Tena ndugu yangu… nitakupa eneo ulime miwa ili upate sukari ya viwandani na ya majumbani, tena nitakupa bure.”
Huyo ni Rais John Magufuli akizindua kiwanda cha kusindika matunda na kuzalisha juisi cha Bakhresa Food Products Ltd kilichoko Mwandege wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.
“Wewe Bakhresa umenifurahisha sana kwa uwekezaji wako; na sukari yako niliyoizuia bandarini, leo (Oktoba 6, 2016) ninamwagiza Waziri (Charles) Mwijage itoke na upatiwe.”
Kauli hiyo ilikuwa ikitoa idhini kwa Bagamoyo Sugar Limited (BSL), kampuni tanzu ya Said Salim Bakhresa (SSBG), kupata ardhi katika Mbuga ya Wanyama ya Saadani, mkoani Pwani.
Hata hivyo, wakati Rais Magufuli anatangaza kutoa ardhi kwa BSL, mwandishi amegundua, hatimiliki Na. 156361MG ya kutwaa eneo mbugani Saadani ilishaandaliwa – tangu tarehe 1 Oktoba 2016, yaani siku tano kabla ya ahadi ya Rais Magufuli. Hati ilitangulia ahadi!
Je, inawezekana rais alikuwa hajui sheria na kanuni zinazotawala mbuga za wanyama? Kanuni Na. 9 ya Kanuni 15 za Usalama za Hifadhi ya Taifa Saadani (SANAPA), inapiga marufuku upandaji mmea wowote ndani ya mbuga hiyo.
Lakini hadi sasa, wazalishaji sukari wameshapanda miwa katika hekta 2,000 kati ya hekta 10,000 walizomegewa hifadhini: Namba ya usajili: 3565-1 na umiliki wa miaka 66.
Msemaji wa Kampuni za Said Salim Bakhresa (SSBG), Hussein Sufian, ambao kiwanda cha sukari ni kampuni yao tanzu, amemwambia mwandishi wa habari hizi kuwa wao walipatiwa eneo hilo kupitia uamuzi binafsi wa Rais Magufuli na wala hawakuomba eneo hilo.
Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009 na Sheria ya Hifadhi za Taifa, Sura 282 (2002), zinazuia kujenga kiwanda na kufanya shughuli zingine za binadamu katika hifadhi za taifa. Lakini BSL imeshajenga kiwanda na inazalisha sukari ndani ya Mbuga ya Saadani.
Utata katika hili ni kwamba, mtoa leseni ya uwekezaji huo mbugani ni serikali – mara hii, hata kwa nguvu ya nyongeza ya kauli ya rais aliyekuwa madarakani.
Vilevile, mmiliki wa Mbuga ya Saadani ni serikali na msimamizi wa utekelezaji wa sheria zinazozuia shughuli kinzani hifadhini ni serikali. Je, serikali au watendaji wake wanafanya makusudi kuvunja sheria na kanuni za hifadhi ya Saadani?
Msemaji wa mwekezaji – SSBG, Hussein Sufian, katika mazungumzo na mwandishi Juni 19 mwaka huu, alisema, “Shida iliyopo ni suala la mpaka. Wizara ya Ardhi wanasema ni wamiliki wa eneo hilo. Wizara ya Maliasili na Utalii wanasema jiwe la mpaka (GN) la hifadhi limepita katika eneo hilo (lao).”
“Sisi (SSBG) hatukuomba eneo (hili). Tulipewa na Rais Magufuli na akaagiza tulime miwa na kuzalisha sukari,” Sufian anasema bila shaka, bila ufahamu wa hoja kuu ya kulinda na kuhifadhi ikolojia ya anakotifua na kuzamisha mbolea yenye kemikali ambazo wataalamu wanaonya huenda zikawa hatarishi kwa viumbe mbugani.
Ardhi walikopewa BSL inahusisha maeneo matano kati ya manane muhimu kwa ikolojia ya SANAPA. Baadhi ya maeneo hayo sasa yanatumika kwa kilimo cha miwa ambayo ni malighafi ya kiwanda cha sukari.
Kinachosikitisha ni kwamba, miaka yote maeneo yaliyotwaliwa kwa kilimo cha miwa, yamekuwa yakitumiwa na wanyamapori kuzaliana. Mengine yamekuwa njia maalum za wanyama (ushoroba), vyanzo vya maji ya Mto Wami na mlango wa maji wanayokunywa.
Vilevile, eneo lililomegwa kwa ajili ya mradi wa kilimo cha miwa na kiwanda cha sukari, lina msitu wa mikoko inayotumika kudhibiti uchafuzi wa mazingira. Eneo hili pia, ni mazalia ya kasa wa kijani – viumbe walio hatarini kutoweka duniani.
Aidha, eneo ililopewa kampuni hiyo ndilo limekuwa linategemewa na wanyamapori kupata maji na malisho wakati wa kiangazi kutokana na asili yake ya kijani kibichi.
Ramani iliyopo inaonesha eneo la hifadhi hiyo linajumuisha Mto Wami, ambao ni maarufu kwa utalii wa boti ili kuona mamba na viboko.
Mbali na kulindwa na Sheria ya Hifadhi za Taifa na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kwa kuwa umo ndani ya Hifadhi ya Taifa, Mto Wami unalindwa na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004, inayozuia kufanya shughuli za binadamu ndani ya eneo la mita 60 toka ukingo wa mto.
Kifungu cha 57(1) cha sheria hiyo kinaelekeza: “Ndani ya mita sitini (60) hakutafanyika shughuli yoyote ya binadamu ya kudumu au ambayo kwa asili inaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi wa mazingira na, au utunzaji wa bahari au kingo za mto, bwawa, au miambao ya asili ya ziwa.”
Haya yote hayakuzingatiwa wakati wa kugawa eneo la Saadani kwa wawekezaji wa kilimo na kiwanda cha sukari – wagawaji wakiwa serikali iliyotunga sheria na kanuni za hifadhi za mbuga za wanyama.
Mwezi Aprili mwaka huu, mwandishi wa habari hizi alihojiana na aliyekuwa Mkuu wa SANAPA, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ephraim Mwangomo juu ya utata huu ambaye alikuwa na maoni haya:
“Bagamoyo Sugar Limited hawana kosa. Makosa yako kwa watendaji wa serikali kutoa kibali cha shughuli za aina hii (kilimo cha miwa na uzalishaji sukari) hifadhini.
“Wao (Bagamoyo Sugar Limited) wamepewa eneo na serikali walime miwa na kuzalisha sukari kiwandani.”
Kamishna Mwangomo, ambaye amehamishwa SANAPA kwenda kuwa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, alitaja shida nyingine iliyoko katika eneo hilo kuwa ni kutokuzingatiwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 wakati wa kumpata mwekezaji na kumega eneo.
Anafafanua, “GN ya hifadhi inajumuisha Mto Wami unaolindwa na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira. Sasa lazima kuwe na utii wa Sheria ya Mazingira.
“Shida nyingine ni kwamba, tembo wanapenda mno miwa. Kulima miwa hifadhini au karibu na eneo lenye tembo ni kuwatia tembo majaribuni ‘for no reason’ (bila sababu). Lile eneo ni ‘part and parcel of their eco-system’ (ni sehemu ya mfumo wao wa kiikolojia),” Kamishna Mwangomo alisema.
Mhifadhi huyo aliongeza: “Tembo wakishaingia katika shamba la miwa, kwa dakika chache tu wanakula miwa mingi, wanaharibu eneo kubwa. Mara nyingi wanatembea wakiwa kundi kubwa. Wale wenye mradi (BSL) wakishawaona tembo, wanatuita, tunawasaidia kuwaswaga.
“Lakini tukumbuke, tembo ni miongoni mwa wanyamapori wenye akili nyingi. Tayari wameshabaini kwamba wakiingia shambani mchana, ni rahisi kushtukiwa. Wamebadili utaratibu, sasa wanaingia shambani usiku.”
SANAPA ina tembo 359 kwa mujibu wa Sensa ya Wanyamapori ya Mwaka 2022.
Kuhusu jinsi ya kumaliza utata huu, Msemaji wa SSBG, Sufian, anasema, wamekuwa na majadiliano na makatibu wakuu wa wizara hizo (Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili na Utalii) tangu miaka mitatu iliyopita.
Anasema serikali, katika kusaka utatuzi wa mvutano huo, iliwataka wasalimishe eneo la mita 500 kutoka ukingo wa Mto Wami kama ilivyoopendekezwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa ajili ya uendelevu wa ikolojia ya Hifadhi ya Saadani.
Hata hivyo, msemaji huyo amesema badala ya kutekeleza hilo, wamekuja na makubaliano mapya yaliyofikiwa na pande hizo mbili; kuwa wazalishaji sukari wasalimishe eneo la mita 200 kutoka ukingo wa Mto Wami na kwa upande wake serikali isalimishe mita 300.
Taarifa za hatua hii ya makubaliano zimethibitishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2021/22. Ripoti hiyo iliwasilishwa bungeni Aprili mwaka huu.
Kuhusu maendeleo, Msemaji wa SSBG amesema katika msimu uliopita, walizalisha tani 18,500 za sukari kutoka hekta 1,200 zilizoendelezwa; kazi iliyofanywa na watumishi 120 wa kudumu na 45 wa msimu. Amesema msimu ujao wanatarajia kuzalisha kati ya tani 35,000 na 40,000 za sukari.
Kwa mujibu wa Sufian, malengo ya kimkakati yaliyopo kwa kampuni hiyo itakapoingia awamu ya tatu ya mradi wake, ni kuzalisha tani 100,000 za sukari kwa mwaka.
Kampuni imewekeza dola za Marekani milioni 110 (Sh. bilioni 265.678) na katika awamu ya tatu, anaeleza Sufian, watapanua uwekezaji hadi dola milioni 300 (Sh. bilioni 724,575).
Katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2020/21, CAG Kichere, alipendekeza serikali na TANAPA kufanya tathmini ya kina kuhusu uhalali na athari za uendeshaji wa mashamba ya miwa na kiwanda ndani ya Hifadhi ya Saadani.
Vilevile, alipendekeza kutafutwe njia bora ya kukabiliana na hali hiyo. Matokeo ya tathmini yawe marejeo kwa matumizi ya baadaye.
Wataalamu wa uhifadhi na utetezi wa ikolojia pamoja na wanaharakati, wanaendelea kupinga shughuli zozote za binadamu katika mbuga za wanyama na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uhifadhi wa mazingira.
*FUATILIA KESHO MADHARA YA KILIMO NA UENDESHAJI KIWANDA HIFADHINI
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED