Alhamisi iliyopita, safu hii ilikuwa na ufafanuzi wa namna matukio ya uvamizi wa wanyamapori katika ardhi ya mkoani Ruvuma. Endelea na simulizi hizo mikoa mingine ya Kusini mwa nchi...
NI asimilia 33 ya ardhi Tanzania, inatajwa kutengwa kwa ajili ya kutunza mifumo ya kiikolojia na mazingira, kuhudumia viumbe, wakiwamo wanyamapori, huku huduma mbalimbali za mazingira zikitolewa hifadhini.
Hivi karibuni kumekuwa kukitokea migongano baina ya binadamu na wanyamapori, hata ikaleta athari kwa binadamu, pia wanyama, ikashia migongano kati yao.
Ni hali inayosababisha watu na maisha mengine kuathiriwa, uharibifu unajitokeza kwa wanyamapori wa maeneo jirani na hifadhi, pia shoroba zao.
Pia, kuna athari za moja kwa moja kwa binadamu, ongezeko la uharibifu wa mali na mazao ikisababisha majeraha kwa wanyamapori, huku kukiwapo matukio ya visasi kwenye hifadhi, kati ya binadamu na wanyamapori; inaishia kujengeka dhana potofu.
Serikali sasa imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Migongano Baina ya Wanyamapori na Binadamu (2020-2024), unaolenga kuboresha maisha ya watu, wanyamapori na haki za jamii kuendelezwa na ustawi wa uhifadhi.
Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, ni miongoni mwa maeneo yenye migongano ya kibinadamu na wanyamapori, sasa serikali inaunda mradi huo.
Ni mpango unaolenga kupunguza migongano ya binadamu na wanyamapori, wadau muhimu wakiboreshewa uwezo wadhibiti na kutatua tatizo hilo.
DC LIWALE
Mkuu wa Wilaya ya Liwale mkoani Lindi Goodluck Mlinga, anataja kinachochangia migongano ya binadamu na wanyama, mojawapo ni eneo kubwa limezungukwa na hifadhi, zikiwamo za Nyerere, Selous na hifadhi za vijiji, jumuiya za hifadhi na maeneo ya uvunaji miti ya mbao.
Anasema maboresho ya uhifadhi wanyamapori yameongezeka kwa kasi; katika vijiji 76, kati yake 64 sasa vina changamoto ya uvamizi wa tembo waliko, pia mashamba yao yakaibua migongano ya binadamu na wanyamapori.
“Wilaya yetu ina jumla ya kilomita za mraba 38,000 na eneo kubwa limezungukwa na hifadhi.
“Tuna hekta zaidi ya milioni 2.5 za uvunaji wa miti ya mbao na tunapata faida kubwa kwenye uvunaji,” anasema Mlinga.
Anataja migongano ya binadamu na wanyamapori imechangia kuwapo miradi ya serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali, yanayowasaidia kumaliza tatizo hilo, ikiwapo serikali ya Ujerumani kupitia Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Katika ulinzi wake hifadhini, GIZ inawasaidia wakazi kukabili changamoto za tembo mashambani mwao, hali inayosababisha migongano na binadamu.
MKAKATI WA KIJERUMANI
Mlinga anataja mkakati wa GIZ kupunguza migongano wameamua kuwasomesha vijana kwenye vyuo vya wanyamapori kutoka vijiji 11, vyenye changamoto kubwa kulinda uhifadhi, vilevile kuwasaidia wananchi kukabiliana na wanyamapori wasifanye uharibifu katika mashamba.
Anasema, mradi wa GIZ uko kutatua changamoto hizo, ikaamua kuja na mbinu nyingine kutoa mizinga ya nyuki kwa vikundi waviweke mashambani, ambako tembo wamekuwa wakiingia, kwani nyuki ni adui mkubwa wa tembo.
Mlinga anataja changamoto nyingine inagusa wafugaji wengi kuvamia misitu, akisema serikali tayari inayatatua kwa kuwatengea maeneo; hekta 42,000 za wafugaji.
MRATIBU MIRADI
Mratibu wa Mradi wa Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori kutoka GIZ wilayani Liwale, Deborah Missana, anasema mradi unatumikia vijiji 11.
Anaviorodhesha kuwa: Turuki, Kitogolo, Mtawatawa, Mtawango, Nahoro, Chimbuko, Nanjegeja, Kimbemba, Naluleo, Ngumbu na Mkutano.
Anasema mradi huo umechagua vijiji hivyo kutokana na changamoto za mgongano kati ya binadamu na wanyamapori, baadhi yao mazao yanaliwa na wanyamapori na wengine wanadhuriwa hasa na Tembo.
Deborah anasema, mafanikio ya mradi huo sasa yapo katika hatua mbalimbali, ikiwamo kuwafundisha wahifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), jumla ya wahifadhi 15; kati yao wanne walitoka wilaya ya Liwale.
Mratibu huyo wa GIZ, anafafanua kuhusu mafunzo hayo kuwa: “Tunakusudia kutumia teknolojia ya kufukuza tembo wavamizi kwa Ndege Nyuki ndio maana tumewapeleka kwenye mafunzo.”
Anaorodhesha mafanikio yanajumuisha kufundisha askari wanyamapori wa vijiji vyote 30 mradi unakopatikana, wakiwamo wasichana 10 na wanaume 20, watakaotoa msaada vijiji humo, pale wanyama waharibifu watakapovamia.
“Pia, tumeweza kutoa mafunzo ya kufundisha Jamii njia ya utatuzi wa Mgongano wa Binadamu na Wanyamapori kwa Lugha ya picha na Michoro ili wenyewe wawe kama wakufunzi kwa wenzao...” anasema mratibu huyo.
Deborah anasema, mafanikio makubwa sasa ni kwa mradi kufanikiwa kufundisha njia mbadala ya utatuzi wa mgongano ya kupika dawa ya harufu ya uzio kufukuza tembo wasiingie shambani.
“Hiii njia ya kupika dawa ya harufu mbaya ya uzio imeonyesha mafanikio kwenye utafiti...” anasimulia na anaongeza:
“Tulianza kufundisha maafisa ugani wa vijiji na baadae kufundisha wana vijiji zaidi ya 1000.”
Mratibu huyo anataja mbinu nyingine, wanawafukuza tembo mashambani kwa mizinga ya nyuki, nayo GIZ imeshatoa mizinga 100 Liwale, hali kadhalika wanatarajia kuongeza 200.
“Hiyo Mizinga itawekwa kwenye mashamba yanayovamiwa na tembo. Wote tunajua tembo na nyuki hawapatani, kwahiyo akifika tu kwenye shamba anakutana na hao nyuki na kuondoka eneo hilo mara moja” anasema Mratibu Deborah.
UZIO UNAONUKA
Ofisa Ujirani Mwema kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kituo cha Selous Liwale, Aloyce Assenga, anasema teknolojia ya kutengeneza uzio wa harufu mbaya waliofundisha wananchi wa vijiji 11 wilayani Liwale, Lindi umezaa matunda.
Anataja katika Pori la Akiba la Selous, limesaidia kufukuza tembo waharibifu wa mazao mashambani, hata ikapunguza migongano ya binadamu na wanyamapori.
Ofisa huyo anaeleza mbinu hiyo imeanza kupunguza wanyama hao na hasa tembo, wanapoona uzio huo wenye harafu inayowasumbua, hivyo wanaamua kutoingia tena mashambani kufanya uharibifu.
Assenga anafafanua kuwa, ni dawa yenye harufu inayowakera wanyama, iliyotengenezwa kupitia mradi shirika la GIZ, mdau mkubwa wa TAWA na sasa umeonyesha matokeo chanya kwenye vijiji hivyo 11.
“Baada ya kutengeneza harufu mbaya kwenye uzio, tulienda kwa ajili ya kupata mrejesho na kiukweli.
“Jamii imeonyesha waziwazi mapokeo chanya kuwa inasaidia kufukuza wanyama wakali hasa tembo katika mashamba” anasema.
Assenga, ambaye pia ni Ofisa Mhifadhi Wanyama Daraja la Kwanza, anataja ushirikiano baina ya TAWA na mradi wa GIZ, wametoa ufadhili wa mafunzo kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji, ili wasaidiane na wale wa TAWA kudhibiti tembo wasiingie mashambani.
Anasema, askari hao wanyamapori vijijini wanapatiwa vifaa zikiwamo mabomu, tochi na pikipiki zinazowasaidia kufika haraka kwenye maeneo yanaripotiwa uvamizi wa wanyama, hata kabla askari TAWA hawajafika.
WATAALAMU KILIMO
Ofisa Kilimo anayeshughulikia mradi wa GIZ wilayani Liwale, Anthony Kawishe, anasema kuwepo changamoto ya uvamizi wa tembo mashambani mwa wakulima, wamekuja na mradi wa kukabiliana na migongano hiyo ya binadamu na wanyamapori.
Anaitaja ni kwa shirika la GIZ, inatoa mafunzo kwa maofisa ugani wa vijiji 11 vya mradi wa namna ya kutengeneza harufu mbaya ya uzio; nao wakatoa mafunzo kwa wananchi vjijini mwao.
Baada ya kufunza, kila kijiji kilitengeneza harufu mbaya ya uzio mashambani na kusaidia maeneo mbalimbali, ikiwamo kwa wakulima wa mpunga, hata tembo waliondoka na hawajarudi tena katika mashamba hayo.
Ofisa Ugani wa Kijiji cha Turuki, Kata ya Mihumo, Liwale Mjini, Yunufu Luwongo, anasema mradi wa GIZ umesaidia kuwatengenezea dawa ya harufu mbaya kwenye Uzio inapowekwa mashambani, yakiwa na ufanisi, tembo hawaingii tena.
Anasema kupitia mradi huo, GIZ imeshatoa mafunzo kwa vijana watatu kwenda katika Chuo cha Askari Wanyamapori wa Vijiji, ili awadhibiti wanyama waharibifu na tayari wameshahitimu na kuanza kazi hiyo katika kijiji hicho.
Mkulima wa Kijiji cha Mtawatawa, Nasoro Gochigochi, anaomba utalaam huo wa kutengeneza uzio wa harufu mbaya uenezwe katika vijiji vingine wilayani Liwale, kwani umeonyesha mafanikio makubwa kuwadhibiti tembo wanaofanya uharibifu.
Askari wanyamapori wa vijiji hivyo waliofunzwa, wakiwamo Radhia Abdallah wa kijijini Turuki, anaomba serikali iwapatie vifaa vinavyowasadia kuimarisha ulinzi vijijini, pia pikipiki inayowawahisha katika eneo la tukio, inaporipotiwa uvamizi wa wanyama mashambani.
Radhia anataja tabia ya tembo, kuwa wakali na wao wanapaswa kuwa na vifaa vya kisasa wanapowafukuza, kutoka wanapovamia mashamba ya wakulima na kufanya uharibifu.
Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari wa Mazingira (JET), John Chikomo, anasema chombo chao kimetoa mafunzo kwa waandishi wa habari na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, namna ya kuripoti kwa usahihi Migongano ya Binadamu na Wanyamapori.
Chikomo anasema, mradi huo unapunguza migongano baina ya binadamu na wanyamapori nchini, ikiwagusa walengwa.
Hao ni wakazi wa vijiji vilivyopo Kusini mwa Hifadhi ya Nyerere na Pori la Akiba la Selous katika wilaya za Liwale Mkoani Lindi, Namtumbo na Tunduru mkoani Ruvuma wakilenga kuboresha uwezo wa wadau nchini wanaohusika na kudhibiti.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED