Vijana waomba ushiriki zaidi masuala ya mabadiliko ya tabianchi

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 05:18 PM Dec 30 2024
Vijana waomba ushiriki zaidi masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
Picha:Mpigapicha Wetu
Vijana waomba ushiriki zaidi masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

LICHA ya tafiti na matokeo ya mikusanyiko mingi kuhusu mabadiliko ya tabianchi duniani kuwataja vijana na watoto kuwa miongoni mwa waathirika wakubwa wa mabadiliko hayo, kundi hilo la kijamii bado linajihisi kutengwa katika vita ya kukabiliana na hali hiyo.

Katika kusanyiko la hivi karibuni katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza lililozungumzia mabadiliko ya tabianchi, baadhi ya vijana waliweka bayana kwamba ni kama dunia na jamii imewatenga katika masuala hayo, huku wao wakitajwa kuwa waathirika wakubwa wa athari zake.

Patrick Michael, mmoja wa vijana walioshiriki warsha hiyo iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Mwanza Youth and Children Network (MYCN), anasema kundi lao ndilo waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi, hivyo kuna umuhimu wa kushirikishwa katika masuala hayo ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na madhara yanayojitokeza.

Kauli yake inaungwa mkono na mwenzake Anna Selemani, ambaye anasema kuwa watoto na vijana ni sehemu ya jamii na kwamba ikiwa watapewa elimu kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi, wana uwezo wa kuisambaza katika jamii.

"Kwa kufanya hivyo, tutasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira hasa ukataji wa miti ovyo na kuchochea upandaji miti ili kuboresha mazingira hasa kwa wazazi wetu," anasema Anna.

Mkazi wa wilayani Magu, Lucy Kennedy, anasema iwapo watoto watashirikishwa katika harakati za kuokoa mazingira kupitia upandaji miti na utunzaji wa mazingira, watafanya vyema kujenga uwezo wao wa kukabiliana na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti ya Hali ya Watoto Duniani (SOWC 2024) iliyotolewa na Shirika la Watoto Ulimwenguni (UNICEF), pamoja na mambo mengine, inabainisha kuwa kutokuwapa kipaumbele watoto katika mikakati ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi kunaweza kuendeleza mzunguko wa vizazi wa umaskini, ukosefu wa usawa, na ustawi duni.

"Serikali na mashirika ya kimataifa lazima yaweke kipaumbele kwa watoto katika sera zinazohusiana na tabianchi, kuhakikisha mahitaji yao ya kipekee na haki zao zinazingatiwa," inasomeka sehemu ya mapendekezo ya ripoti hiyo iliyozinduliwa Novemba 2024.

Katika kusanyiko la wilayani Magu ambalo pia lilijumuisha wanafunzi wa Shule ya Sekondari Lugeye, Mratibu wa Mwanza Youth and Children Network (MYCN), Ester Kusekwa, alisema vijana wakiwezeshwa wanaweza kuwa mabalozi wazuri katika masuala ya utunzaji wa mazingira, kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa.

"Uchafuzi wa mazingira ni hatari, unachangia athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo pia zinasababisha milipuko ya magonjwa ambayo yanaweza kusababisha vifo na kupoteza nguvu kazi ya taifa," anaeleza Kusekwa na kuongeza:

"Ili dunia iendelee kuwa salama, ni lazima kila mwananchi ndani ya jamii ahakikishe anatunza mazingira vizuri kwa kufanya usafi katika eneo lake analoishi na kupanda miti ya kutosha."

1

Ripoti ya Hali ya Watoto Duniani (SOWC 2024) pia inataja madhara ya kiafya kama moja ya athari za mabadiliko ya tabianchi, hasa kutokana na uchafuzi wa hewa, magonjwa yanayosababishwa na maji, na utapiamlo ambavyo vinazidi kuenea.

"Watoto, hasa walio chini ya umri wa miaka mitano, wako hatarini zaidi na wanakabiliwa na viwango vya juu vya vifo na maradhi," inasomeka sehemu ya ripoti hiyo iliyotolewa na UNICEF.

Katika warsha ya Magu, pamoja na mambo mengine, vijana walifundishwa mbinu bora za kuchangamkia fursa za kiuchumi, kukuza uzalendo, na kuimarisha utunzaji wa mazingira, kwa lengo la kuwa kizazi kinachochochea mabadiliko chanya.

Mohamedi Mpoto, ambaye ni Ofisa Wanyamapori, akitoa elimu kuhusu mazingira, alisema mazingira bora ni muhimu katika maendeleo ya vizazi vya sasa na vijavyo, hivyo vijana wanapaswa kuzingatia mbinu za kujilinda na kujikinga dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Ushirikishwaji wa watoto na vijana katika vita dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi ni suala ambalo linapewa msukumo na taasisi mbalimbali, zikiwemo Shirika la WeWorld ambalo limekuwa likitekeleza miradi kadhaa shirikishi inayolenga kusaidia utunzaji wa mazingira.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ule wa Kijani Pemba unaotekelezwa Kisiwani Pemba, ukilenga kuboresha hali ya maisha ya watu binafsi na familia katika maeneo makuu ya mijini kwenye Kisiwa cha Pemba, kwa kuzingatia upatikanaji wa huduma, usafi, huduma za umma, usimamizi wa taka, upangaji wa miji endelevu, na masuala yanayohusiana na jinsia.

Akizungumza na Nipashe, Meneja wa mradi wa Kijani Pemba, Francesco Paris, anaeleza kuwa upungufu katika upatikanaji wa chakula, maji, huduma za afya, elimu, na ushiriki mdogo wa watu katika suala zima la mazingira ni changamoto inayohitaji utatuzi.

"Hivyo, sisi WeWorld tunafanya vitu mbalimbali ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kutoa elimu kwa jamii hasa kwa vizazi vipya kuhusu mazingira, namna ya kuyalinda, kuyatunza, na kuwapa mbinu za kudhibiti uchafuzi wa mazingira na hali ya hewa," anasema Paris na kuongeza:

"Kutokana na mvua zisizotabirika, tunatekeleza mradi wa kilimo ambao unahamasisha matumizi ya kiasi kidogo cha maji pia jinsi ya kukabiliana na mmomonyoko wa ardhi, ambalo linaweza kuwa tatizo kubwa. Katika hili, tunatoa elimu kwa jamii isikate miti hovyo ili kuilinda ardhi kuwa imara na tunahamasisha upandaji wa miti," anasema Paris.

"Kwa upande wa Pemba, tuna mradi wa biashara ya kijani ambapo tunatoa elimu ya namna ya kufanya biashara. Pia, tunatoa ufadhili kidogo kwa wenye andiko zuri la mradi wa biashara na wa mazingira kwa ajili ya kufanikisha shughuli zao," anasema Paris.

Anaongeza kuwa ufadhili wa miradi ya mazingira unatokana na ukweli kwamba zipo athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza kwenye suala zima la mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo msukumo wa juu wa damu (high pressure), kichwa kuuma, na kiwango kikubwa cha joto.

Ripoti kadhaa zinaonyesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yana athari kubwa hasa kwa makundi ya watoto na vijana kuliko ilivyo kwa watu wazima.

Miongoni mwa ripoti za karibuni kabisa ni ile ya SOWC 2024 inayobainisha kuwa ipo haja ya kuchukua hatua za kukabiliana na matukio hatari yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi kwani watoto zaidi ya bilioni moja barani Afrika wanaishi katika maeneo yenye athari za mabadiliko ya tabianchi kama mafuriko, ukame, na mawimbi ya joto.

Kadhalika, ripoti hiyo inataja hali hiyo kusababisha madhara ya kiafya yanayotokana na uchafuzi wa hewa, magonjwa yanayosababishwa na maji, na utapiamlo vinavyozidi kuenea. Eneo jingine linaloathiriwa ni changamoto za elimu.

"Majanga ya asili yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi tayari yanapelekea kufungwa kwa shule, kupunguza upatikanaji wa elimu, na kuathiri fursa za muda mrefu kwa watoto walioathirika," inasomeka sehemu ya ripoti hiyo ya SOWC 2024 na kuongeza:

"Pia kuna athari za kisaikolojia ambazo ni watoto kupatwa na msongo wa mawazo unaotokana na kuhama makazi, kupoteza mali, na hali ya kutokuwa na uhakika kwa sababu ya majanga ya tabianchi. Hali hiyo inachangia wasiwasi, unyogovu, na changamoto nyingine."