Mwana FA apagawisha Usiku wa Singeli NMB Day

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:44 AM Aug 23 2024
Naibu Waziri Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma 'Mwana FA' akitumbuiza wakati wa Usiku wa Singeli wa NMB katika Tamasha la Kizimkazi.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Naibu Waziri Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma 'Mwana FA' akitumbuiza wakati wa Usiku wa Singeli wa NMB katika Tamasha la Kizimkazi.

NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Khamis Mwinjuma “Mwana FA”, amepagawisha mashabiki waliohudhuria Usiku wa Singeli wa Siku ya Benki ya NMB ‘NMB Day’ katika Tamasha la Kizimkazi, ambako alitumbuiza kwa dakika 10.

Usiku wa Singeli ulikuwa hitimisho la NMB Day, siku maalum iliyotumika kukabidhi na kuzindua miradi iliyotekelezwa na NMB katika Kizimkazi Festival, ambako ilikabidhi Skuli ya Maandalizi kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na kung’arishwa na bonanza la michezo.

Mgeni rasmi wa Usiku wa Singeli alikuwa ni Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulid Mwita.

 Mwana FA, nyota Hip Hop wa lililokuwa Kundi la East Coast Team, alipanda jukwaani saa 3:45 usiku, ambapo alianza kutoa hotuba fupi kabla ya mashabiki kumshawishi atumbuize, ndipo alipoanza michano ya kibao chake cha Habari Ndio Hiyo, Unanijua Unanisikia.

Baada ya mistari michache ya Unanijua Unanisikia, MwanaFA akadondosha ‘vesi’ moja ya kibao chake kiitwacho Mfalme alichomshirikisha G Nako, kabla ya kugeukia singeli na kuchana ‘free style’ kali na kumalizia kibao cha Sio kwa Ubaya alichoimba na Harmonize.

“Nimshukuru Waziri Tabia kunichagua kuambatana nami hapa, niwashukuru marais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan na Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kazi kubwa wanayofanya kuipambania sanaa ya Tanzania, ambayo inapaswa kupambaniwa pia na wasanii wenyewe," alisema Mwana FA.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwan Kikwete, ndiye aliyekabidhi vikombe kwa washindi wa bonanza hilo lililohusisha michezo ya karate, bao la kete, karata, kufua na kukuna nazi na kuvuta kamba.