Dube, Azam wamalizana rasmi, huru kutua kokote

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 10:51 AM Jun 28 2024
Mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube.
Picha: Mtandao
Mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube.

MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Prince Dube, amelipa kiasi cha Dola za Marekani 200,000 kwa klabu hiyo ili kuvunja mkataba na kuanza mchakato wa kujiunga na timu nyingine, imefahamika.

Uongozi wa Azam ulimtaka mchezaji huyo au klabu inayomtaka kulipa kiasi cha Dola za Marekani 300,000 ili kuvunja mkataba uliokuwapo.

Lakini baada ya klabu hiyo ya Chamazi kutoa tamko hilo, pande hizo mbili zilikutana kufanya mazungumzo na hatimaye Dube alitakiwa kulipa kiasi hicho alichoweka benki ili kuwa mchezaji huru.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana, zinasema mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe alilipa kiasi hicho cha fedha tangu wiki iliyopita na sasa hivi Azam FC inasubiri kuona muamala huo umeingia kwenye akaunti yao.

Chanzo chetu kimesema uongozi wa Azam umethibitisha kupokea viambatanisho vya malipo hayo lakini wanasubiri kuzipokea rasmi ndani ya akaunti yao.

"Ni kweli Dube alifanya malipo ya Dola 200,000 na kuwasilisha karatasi halisi za malipo hayo kwa uongozi wa Azam, lakini kama unavyojua taratibu za fedha na kibenki, pesa hiyo bado kwetu haijasomeka.

Mara baada ya kuzipokea, tutaweka wazi kama ambavyo tulifanya wakati wa nyuma mchezaji wetu alipoonyesha nia ya kutaka kuondoka kwenda kujaribu changamoto mpya," kilisema chanzo chetu.

Habari zinasema Dube anatarajia kujiunga na mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga na ndio waliofanikisha mchakato huo kumalizika mapema.

Klabu hiyo pia inatajwa kugharamia ziara ya mapumziko ya mshambuliaji huyo nchini Ufaransa.