TIMU ya Kipanga FC inatarajia kuikabili New City FC katika mechi ya Ligi Kuu Zanzibar itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Mau, visiwani hapa.
Kocha Mkuu wa Kipanga FC, Hassan Khamis, aliliambia gazeti hili anatarajia mechi hiyo itakuwa ngumu kwa pande zote mbili.
Khamis alisema amewaandaa wachezaji wake kucheza kwa umakini na utulivu kwa sababu kwa sasa wanahitaji zaidi pointi tatu ili kujiondoa katika nafasi waliyoko kwenye msimamo wa ligi hiyo.
"Hatutaki kufanya makosa katika mchezo huu wa kwanza katika mzunguko wa pili, ninawakumbusha wachezaji kukifanya kile tunachokifanya kwenye uwanja wa mazoezi. Tumefanya maboresho mengi katika kipindi chote cha mapumziko ya ligi, tumefanikiwa pia kupata maingizo mapya kulingana na mahitaji yetu,” alisema kocha huyo.
Aidha alisema katika mchezo huo anatarajia kuwatumia wachezaji watano wapya ambao wamejiunga na timu hiyo wakati wa dirisha dogo la usajili ambao anaamini watakiongezea nguvu kikosi chao.
Kipanga FC yenye pointi 17 inateremka uwanjani ikiwa ipo katika nafasi ya 12 na wakati wapinzani wao New City wenye pointi 12 wako nafasi ya 14 katika msimamo wa hiyo ya juu Zanzibar.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED