Malindi yaachwa wachezaji 14

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 07:04 AM Jun 27 2024
Malindi SC.
Picha: Mtandao
Malindi SC.

BAADA ya kufanya vibaya katika msimu uliomalizika, uongozi wa Malindi SC umesema hawataki kurudia makosa na wamejipanga kukamilisha mapema mchakato wa usajili.

Malindi ilimaliza katika nafasi ya 10 ikiwa na pointi 36 katika msimu uliomalizika wa 2023/2024, wakishinda michezo 10, sare ya  sita na imefungwa michezo 14.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Malindi, Suleiman Mohamed ‘Kocha Mo’ alisema wameanza na uamuzi wa kuwaacha wachezaji 14 ambao walikuwa katika kikosi cha msimu uliomalizika.

Kocha huyo alisema wanajipanga kufanya usajili 'mkubwa' ambao utawapa matokeo chanya na hatimaye kurejesha makali yao katika Ligi Kuu Zanzibar msimu ujao.

"Tunafanya maboresho mapema katika kikosi chetu, tumeona hatukuwa na msimu mzuri, hatukuwa bora sana, tulibakia kupambana ili kuibakisha timu Ligi Kuu, msimu ujao tunataka turejee kivingine," alisema kocha huyo.

Hata hivyo aliongeza msimu uliopita ligi ilikuwa na ushindani na hakukuwa na mechi rahisi na hiyo imesaidia kuchelewa kupatikana kwa bingwa na timu zilizoshuka daraja.

"Tulikosa washambuliaji wazuri, eneo hili lilikuwa ndio changamoto zaidi katika upande wetu, sasa tunalitupia macho kwa ukubwa katika kusaka wachezaji wenye uwezo," aliongeza.