Mashabiki Simba SC, Yanga wafunguka nguvu ya Chama

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 07:58 AM Jun 27 2024
Clatous Chama.
Picha: Mtandao
Clatous Chama.

WAKATI bado haijawekwa hadharani, Clatous Chama, ataitumikia klabu ipi katika msimu ujao wa mashindano, mashabiki wa Simba na Yanga kutoka sehemu mbalimbali nchini, wametoa maoni yao kuhusiana na kiungo huyo raia wa Zambia.

Chama amebakiza siku tatu tu katika mkataba wake na Wekundu wa Msimbazi.

Akizungumza jijini jana, shabiki wa Yanga, Azizi Kalinga, alisema kiungo huyo ni mmoja wa wachezaji wenye uwezo mkubwa kwa sasa na hakuna timu ambayo ikifanikiwa kumpata itajutia usajili huo.

Kalinga alisema mchezaji huyo ana uzoefu na amekuwa akisaidia timu yake kupata matokeo muhimu na hiyo inatokana na kipaji alichonacho.

"Sisi tumejipanga na tumekamilika, tuna uwezo wa kumpata mchezaji yoyote tunayemhitaji hapa Tanzania, hatutamkosa, iwe Clatous Chama au Prince Dube, hatuwezi kushindwa kumsajili ," alisema shabiki huyo.

Amri Diaz, alisema anaamini walifanikiwa kumnasa Chama, kikosi chao kitakuwa imara na kitatoa 'dozi' kwa kila watakayekutana naye.

"Naona kabisa kuna mtu atakula 10 msimu ujao, huku Chama huku Dube, tutakuwa na kikosi tishio Afrika, tunaamini hakuna atakayeweza kututisha, hakuna atakayeingia mguu wake akatoka salama," alitamba shabiki huyo wa Yanga.

Aliongeza lengo la Yanga kusajili wachezaji mbalimbali ambao ni mahiri na wazoefu ni kutaka kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kufanya vyema kwenye mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Naye mwanachama wa Simba, Fadhila Juma, alisema bado Chama ni mchezaji muhimu ambaye anahitajika ndani ya kikosi chao.

Alisema kumwacha Chama kwa sasa hautakuwa uamuzi wa busara kwa sababu timu yao inahitaji kuimarishwa katika idara zenye mapungufu.

"Kumwacha Chama si uamuzi mzuri, kwa upande wangu naona bado ana nafasi na mchango mkubwa katika kikosi chetu, kwa sasa unaweza kuleta mtu mpya, je kama atashindwa kuonyesha uwezo wake au kuingia katika mfumo itakuaje, itaigharimu timu," alisema shabiki huyo.