Nyota Yanga sasa kumtesa Gamondi

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 07:16 AM Jul 02 2024
Kocha Miguel Gamondi.
Picha: Mtandao
Kocha Miguel Gamondi.

MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Yanga jana ilitangaza kumsajili mchezaji wa zamani wa Simba, Clatous Chama, ambaye ataichezea timu hiyo msimu ujao kwenye Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Usajili huo unatajwa kuwa mtihani kwa kocha Miguel Gamondi katika kuamua nani aanze kwenye kikosi hicho ambacho sasa kitakuwa na wachezaji watatu wenye uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo wa kati na mshambuliaji namba 10.

Kabla ya kusajiliwa kwa Chama, Gamondi amekuwa na nyota watatu wenye uwezo mkubwa wa kucheza namba hizo, ambao ni Max Nzengeli, Aziz Ki na Pacome Zouzoua ambao wamekuwa wakimpa matokeo chanya kwenye michezo mbalimbali.

Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, aliliambia Nipashe jana kuwa uongozi umekamilisha usajili wa Chama na sasa kazi imebaki kwa Gamondi kukuna kichwa kuamua nani atakuwa anaanza kati ya nyota hao.

"Tunaamini ni usajili wenye tija, kuna kitu kinaenda kuongezeka kwenye kikosi, hapa kazi ipo kwa kocha na ni mtihani kwake katika kuamua nani aanze na kwenye nafasi gani, tunataka Yanga iwe bora zaidi ya msimu uliopita," alisema kiongozi huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe.

Usajili huo wa Chama ndani ya Yanga sasa utamfanya kocha Gamondi kuwa na machaguo mengi kwenye nafasi ya mshambuliaji namba 10 na kiungo wa kati ingawa Mzambia huyo pia ana uwezo wa kucheza kama mshambuliaji anayetokea pembeni kama ilivyo kwa Pacome.

Chama amejiunga na Yanga baada ya tetesi za muda mrefu, Mzambia huyo alimaliza mkataba wake wa kuichezea Simba Juni 30, mwaka huu na kuwa huru kujiunga na timu yoyote.

Mzambia huyo amesaini mkataba wa mwaka mmoja huku ikitajwa kupewa dau kubwa la usajili na anakuwa mchezaji mwingine katika kundi la wachezaji wachache wa kimataifa kuzichezea Klabu za Simba na Yanga.

Baadhi ya wachezaji waliochezea timu hizo kwa nyakati tofauti katika kipindi cha hivi karibuni ni Ramadhan Waso, Mike Barasa, Emmanuel Okwi, Amissi Tambwe, Hamis Kiiza, Haruna Niyonzima, Benard Morrison na Saido Ntibazonkiza.

Inaelezwa Chama aliugawa uongozi wa Simba katika kufanya maamuzi ya kumuongezea mkataba au kuachana naye ili kusajili mchezaji mwingine.

Mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya klabu hiyo ya Simba anasema uongozi wa klabu hiyo uligawanyika ambapo wapo ambao walitaka nyota huyo asiongezewe mkataba kwa kuwa kiwango chake kimeisha na amekuwa msumbufu, lakini wapo waliotaka nyota huyo kuongezewa mkataba.