Rais ZFF asifu Z'bar kusheheni vipaji vya soka

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 07:36 AM Jul 02 2024
RAIS wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Dk. Suleiman Mahmoud Jabir.
Picha: Mtandao
RAIS wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Dk. Suleiman Mahmoud Jabir.

RAIS wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Dk. Suleiman Mahmoud Jabir, amesema Zanzibar imejaliwa vipaji vingi vya soka ambavyo huhitaji kuvitafuta bali kinachohitajika ni kuvilea na kuviendeleza.

Hayo aliyaeleza alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Mao Zedong B, baada ya kumaliza ufunguzi wa mashindano ya akademi za vijana yanayoendelea visiwani hapa.

Alisema ni jambo la kufurahisha na kuona kuwa wana waalimu ambao wamewakusanya vijana hao kwa ajili ya kuvitunza na kuvilea vipaji hivyo.

“Lakini pia nishukuru kuona mashindano ni ya akademi lakini pia na umri uliopo, hivyo unaweza kuona kwamba kuna vipaji vinatafutwa, vinalelewa na kuendelezwa,” alisema.

Sambamba na hayo alichukuwa fursa hiyo kutoa shukrani zake  kwa wazazi wa watoto hao kwa kuona umuhimu wa uwapo wa mashindano hayo na  kuhakikisha yanafanyika.

Katika mashindano hayo ambayo yameandaliwa na Akademi ya YFDA, yanashirikisha watoto chini ya miaka 10, 14, 16 na 20 na hii ni mara ya pili kufanyika kwake na mara ya mwisho yalifanyika mwaka jana.

Mashindano ya Zanzibar Akademi 2024 yanashirikisha akademi 11 zilizotoa timu 20, zikiwamo Akademi ya Small Simba, Mamboul, New Boys, All Star, Korosini City, JKU, Mkokotoni, Muyuni, Beitras na wenyeji YFDA.