Sekilojo ashauri mambo 4 Yanga

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:41 AM Jun 28 2024
Sekilojo aishauri Yanga.
Picha: Mtandao
Sekilojo aishauri Yanga.

WAKATI Yanga ikiwa katika dakika za mwisho za kumnasa mshambuliaji wa zamani wa Medeama FC ya Ghana, Jonathan Sowah, aliyekuwa mchezaji nyota wa timu hiyo na Taifa Stars, Sekilojo Chambua, ameanika mambo manne muhimu ambayo mabingwa hao wanatakiwa kufanya ili kuwa na kikosi tishio kuelekea msimu mpya wa mashindano.

Akizungumza na gazeti hili jana, Chambua alisema ili Yanga iendeleze makali yake katika mashindano ya ndani na ya kimataifa watakayoshiriki msimu ujao, inatakiwa kuboreshwa kwenye eneo la beki wa kati, eneo la mshambuliaji wa kati na winga.

Chambua alisema kama Yanga itaongeza nguvu katika maeneo hayo, anaamini itakuwa na nafasi ya kufika mbali kwenye mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

"Kocha wetu Gamondi yeye anafahamu zaidi nini cha kufanya kukiongezea ubora kikosi chetu, lakini mimi nadhani tunapaswa kuongeza mshambuliaji mmoja wa kati mwenye uwezo mkubwa, winga mwenye damu changa lakini uwezo mkubwa pamoja na beki mmoja wa kati kwa ajili ya kuja kuwasaidia Dickson Job na Bacca (Ibrahim Hamad)," alisema Sekilojo.

Alisema Yanga pia wanapaswa kutafuta golikipa mwingine kwa ajili ya kumsaidia Djigui Diarra, kipindi hiki ambacho Metacha Mnata ameondoka ndani ya timu hiyo.

"Sijajua Yanga wamefikia wapi na Mshery (Abdultwalib), kwa sababu nimesikia amemaliza mkataba, lakini bado kuna haja ya kuongeza kipa mwingine kwa ajili ya kumsaidia Diarra," alisema nyota huyo.

Aliongeza wapo wachezaji ambao wataachwa na timu hiyo kwa kufuata uamuzi wa Gamondi, hivyo viongozi watumie nafasi hizo kuongeza wachezaji watakaokuwa na mchango mkubwa kwa timu.

Habari zilizopatikana jijini kutoka ndani ya Yanga zinasema Sowah ambaye kwa sasa anaitumikia Al Nasr Benghazi ya Libya anakuja kuchukua nafasi ya Joseph Guede ambaye huenda akaondoka ndani ya kikosi hicho kilichoko chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.

Chanzo hicho kiliendelea kusema mazungumzo kati ya Yanga na mchezaji huyo yamemalizika na sasa wameanza mchakato wa kumalizana na klabu yake kwa sababu bado ana mkataba.

"Viongozi wameonekana wanamhitaji, hasa baada ya yeye kutokuwa na furaha na timu hiyo (Al Nasr), alijiunga nayo Januari, mwaka huu lakini anataka kuondoka, uzuri mchezaji mwenyewe amekuwa na mahusiano mazuri na uongozi wetu baada ya kufahamiana tulipocheza mechi mbili za mashindano Ligi ya Mabingwa Afrika, na ilikuwa kidogo asajiliwe kipindi cha dirisha dogo, lakini ikashindikana akaenda Libya," kilisema chanzo hicho.

Medeama ilikuwa Kundi D pamoja ya Yanga katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliomalizika na mchezaji huyo alionekana akiisumbua safu ya ulinzi ya Gamondi katika mechi zote mbili, akifunga bao la penalti katika mchezo wa kwanza uliyochezwa Desemba 8, mwaka jana huko Ghana, timu hizo zikitoka sare ya goli 1-1, na alikosa tuta katika mechi ya pili iliyochezwa nchini, baada ya wiki mbili, wenyeji wakishinda mabao 3-0.

Chanzo kingine kilisema Yanga iko katika mipango ya kumsajili kiungo mkabaji chipukizi, Mtasigwa, ambaye amepata makuzi mazuri ya soka lake nchini Iceland na kabla ya kujiunga na Azam msimu wa 2023/2024.

"Alituvutia sana hasa kwenye mechi anazocheza katika kikosi cha Stars, na 'tulimvulia kofia' kiwango alichoonyesha katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA pale New Amaan Complex (Zanzibar) ingawa Yanga ilitwaa ubingwa," kiliongeza chanzo chetu.

Yanga pia inatajwa inahitaji kumsajili kiungo mkabaji wa Azam FC na Taifa Stars, Adolf Mtasigwa.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema jana hawawezi kuzungumza lolote kuhusu usajili kwa sababu bado wako mapumzikoni baada ya kazi ngumu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la FA na kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Jamani tuacheni kwanza tule bata, kazi ilikuwa ngumu, kwa sasa tupo mapumzikoni, subirini kuanzia Julai Mosi kila kitu tutaanza kukiweka hadharani," alisema Kamwe.

Hatimaye Yanga imeondolewa kifungo cha kusajili baada ya kumalizana na aliyekuwa mchezaji wao, Lazaraus kambole, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), limesema jana katika taarifa yake.

Yanga sasa pia itakuwa huru kufanya usajili wa ndani.