Serikali yazitaka Yanga, Simba kufanya usajili mzuri kimataifa

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:51 AM Jun 27 2024
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa.
Picha: Mtandao
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa.

SERIKALI imezitaka klabu zitakazoiwakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa zikiwamo Yanga na Simba kufanya usajili mzuri, makini na wa kiufundi, ili kufanya vyema kwenye michuano hiyo.

Mbali na klabu hizo, pia Azam FC na Coastal Union nao watashiriki michuano hiyo ya kimataifa ambapo Yanga na Azam zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Coastal Union zenyewe zitashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi jioni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema kufanya vizuri kwa timu hizo kwenye michuano hiyo ya kimataifa kutatokana na usajili wenye tija watakaoufanya.

"Mimi nikizungumza kwa niaba ya serikali nazitaka Simba na Yanga zijiandae vizuri tunazitakia kila la heri, lakini zifanye usajili mzuri ili ziende kuiwakilisha vyema nchi, zifike hatua kama za msimu uliopita au zaidi, tunaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuhakikisha kwamba ushiriki wetu unakuwa wa kimkakati na siyo kusindikiza watu wakatufunge," alisema Msigwa.

Alisema ana uhakika timu zote, hata Azam na Coastal Union ambazo nazo zitacheza michuano ya kimataifa zitafanya vyema kwa sababu ligi ya Tanzania kwa sasa ni nzuri, hivyo timu zote zilizofuzu ziende kuleta ushindani mkubwa.

"Timu ziendelee kupeperusha bendera ya nchi na kama kawaida bao la mama litakuwapo kuanzia hatua kama ya msimu uliopita, kilichobaki wafanye usajili mzuri, waziandae timu vizuri, serikali iko nyuma ya timu zote," alisema Msigwa.

Aidha, alisema serikali itafunga kifaa cha kuwasaidia waamuzi (VAR) kwenye viwanja vipya itakavyojenga, Arusha na Dodoma.

"Tumefanya tathmini ya kutumia video ya kuwasaidia waamuzi VAR, Uwanja wa Benjamin Mkapa una uwezo wa kufungwa,  viwanja vipya vya kisasa vitakavyojengwa Arusha na Dodoma navyo tutafunga vifaa hivyo, lakini wakati tunavikarabati viwanja vyetu vilivyopo sasa tutazingatia kuweka maeneo ya kufungwa miundombinu hiyo, hilo halina wasiwasi na serikali imeshaondoa kodi ya vifaa hivyo," alisema Msigwa.