Simba kushusha silaha tatu mpya

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:45 AM Jun 28 2024
Kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ohoua.
Picha: Mtandao
Kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ohoua.

WEKUNDU wa Msimbazi wako katika hatua za mwisho za kuwasajili nyota wapya watatu ambao wanatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote ili kukamilisha taratibu za kujiunga na Simba, ikiwamo kufanya vipimo vya afya.

Wachezaji hao ambao wanatajwa kukaribia kujiunga na Simba ni pamoja na kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ohoua, mwenye umri wa miaka 22 kutoka Stella Adjame ya Ivory Coast, kiungo mkabaji, Debora Mavambo, ambaye anaichezea Mutondo Stars ya Zambia na beki wa kushoto, Valentin Nouma kutoka Rahimo FC.

Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya Simba zinasema wachezaji hao walishafikia makubaliano ya awali na kilichobakia ni kukamilisha taratibu za mwisho baada ya kutua nchini.

Kiliongeza pia nyota wote wapya waliosajiliwa na Simba wanatakiwa kuwasili Dar es Salaam Julai Mosi ili kuendelea na maandalizi ya safari ya kuelekea Morocco ambapo wanaenda kuweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya.

Kilisema pia nyota hao watapiga picha rasmi zitakazotumika katika zoezi la utambulisho.

"Ohoua ndiye mchezaji bora wa msimu wa 2023/2024 nchini Ivory Coast, anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, amehusika na mabao 21 (amefunga magoli 12 na asisti tisa), sasa nikwambie tu huyu mchezaji amesajiliwa rasmi kuchukua mikoba ya Clatous Chama, huyu ndiye atauzika ufalme wake, viongozi wamefikia uamuzi wa kuleta 'mashine' mpya kwa sababu jamaa (Chama), umri umekwenda halafu amekuwa msumbufu, ili tumfanye atulie ni kumletea mtu kama yeye au zaidi yake," kilisema chanzo hicho kutoka Msimbazi.

Chanzo hicho kiliongeza, Mavambo ambaye anacheza Ligi Kuu Zambia anatajwa kuwa ni mmoja wa wachezaji wanaotarajiwa kumaliza tatizo la kiungo mkabaji katika kikosi cha Simba.

"Huyu ana umbile kubwa, alivyo kama Khalid Aucho au Thadeo Lwanga, sehemu iliyokuwa inatusumbua sana Simba kwa muda mrefu ni ya kiungo mkabaji, huyu ni mmoja wa wanaokuja kuziba pengo, huku nyuma nilikwambia kuna mbadala wa Mohamed Hussein, anakuja, mambo yamekamilika, nadhani wiki hii Valentin atakuja kwa ajili ya vipimo vya afya na kusaini mkataba wa miaka mitatu, ni kijana mdogo ana miaka 23 tu," kiliongeza.

Wakati huo huo, habari zinasema winga msumbufu, Mutale, raia wa Zambia ameshawasili nchini akiwa na familia yake tayari kwa kusaini mkataba wa kuitumikia Simba.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amekiri wachezaji wapya watakaovaa jezi ya klabu hiyo katika msimu mpya watawasili wakati wowote kuanzia wikendi hii.

"Nilisema na nitaendelea kusema, safari hii hatufanyi mzaha, tunafanya usajili mkubwa, na tutaachana na wachezaji wengi watapewa 'thank you', wapo tutakaoachana nao kwa kumaliza mikataba na wengine tutaivunja, lengo ni kupata wachezaji wenye viwango bora," Ahmed alisema.