WAKATI kikosi cha Simba kikitarajiwa kuwasili Tabora mapema leo, uongozi wa timu hiyo umesema umekwenda mkoani humo kwa lengo moja la 'kulipiza kisasi' kufuatia wenyeji Tabora United kuzifunga timu nyingine za Dar es Salaam walipokutana katika mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara, imeelezwa.
Tabora United inatarajia kuikaribisha Simba katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mbali na kuhitaji ushindi, 'kuzilipia' kisasi timu zote za Dar es Salaam ni moja ya kilichowapeleka Tabora.
Ahmed alisema hawahofii chochote kuelekea mchezo huo, badala yake wamedhamiria kuchukua pointi tatu muhimu na kujiimarisha kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo.
"Kwanza tunakwenda kuzilipia kisasi timu zote za Dar es Salaam ambazo zimeonewa na Tabora United, haiwezikani timu ya Dar es Salaam ikafanywa mnyonge, kwa hiyo tunakwenda kumlipia kila Mwana-Dar es Salaam ambaye alidhuriwa katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu. Ni jukumu la timu zote kutuunga mkono, kukaa nyuma yetu ili tumshikishe adabu," alisema Ahmed.
Aliongeza mchezo huo hautakuwa rahisi kutokana na Tabora United kujiamini, lakini wao pia wanamatumaini kutokana na ubora wa kikosi cha benchi lao la ufundi kiinachoongozwa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids.
"Haitakuwa mechi rahisi, ni ngumu kwa sababu Tabora United inaonekana baada ya kupata ushindi dhidi ya timu za Dar es Salaam, imejenga kujiamini sana, tuseme pia ni timu nzuri, lakini amezifunga timu anazofanana nazo.
Uwezo wake wa kupata ushindi ni kwa timu inayoshika nafasi ya pili kushuka chini, kuna baadhi ya watu wanasema eti tunakwenda kucheza ugenini sisi hatuna ugeni, kumbuka msimu uliopita pale pale tuliwakung'uta mabao 4-0, popote sisi tunakanyaga na popote kambi," Ahmed alitamba.
Tabora United iliifunga Yanga mabao 3-1, mechi iliyochezwa Novemba 7, mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex halafu ikapata ushindi mwingine wa ugenini magoli 2-0 dhidi ya KMC na Desemba 13, mwaka jana ikawachapa Azam FC mabao 2-1, nyumbani kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Simba itashuka uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi mnono wa mabao 4-0, katika mechi ya mzunguko wa pili msimu uliopita, shukrani ziende kwa Pa Omar Jobe, Sadio Kanoute, Che Malone Fondoh na Fred Koublan, kwa kupachika wavuni magoli.
Ikumbukwe vinara hao walipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Agosti 17, mwaka jana kwenye Uwanja wa KMC Complex, Che Malone, Valentino Mashaka na Awesu Awesu, wakifunga.
Rekodi pia zinaonyesha kuwa msimu huu, Simba haijapoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu, ikicheza ugenini, badala yake imeshinda zote, huku sare moja ya mabao 2-2 iliyoipata dhidi ya Coastal Union na kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Yanga, vyote ilikuwa kwenye michezo yake ya nyumbani.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED