Singida Black Stars yarejea nyumbani, yaitisha Kagera

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:48 AM Feb 01 2025
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza.
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza.

WAKATI hatima ya nyota wake watatu waliopewa uraia wa Tanzania ikiwa bado chini ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), kikosi cha Singida Black Stars kimerejea mkoani, Singida tayari kuisubiri Kagera Sugar, imeelezwa.

Singida Black Stars iliweka kambi jijini Arusha lakini imelazimika kuvunja kambi hiyo kutokana na mabadiliko ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inatarajia kurejea tena kuanzia leo.

Matajiri hao wa asali wataikaribisha Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Liti, huku uongozi wakisema wachezaji wote waliosajiliwa  dirisha dogo wamekamilisha taratibu za usajili.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, amesema licha ya uchovu wa safari, kikosi chao kilichoko chini ya Kocha Mkuu, Hamdi Miloud, mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa, kiko tayari kwa mzunguko wa pili.

 "Tumewasili nyumbani baada ya kukaa kambi ya majuma kama matatu hivi, wachezaji wamechoka sana kwa hiyo tunawapa mapumziko mafupi, wamefanya kazi kubwa sana kule Arusha kujiandaa, watapumzika kwa siku mbili, baada ya hapo tutarudi kwenye uwanja wa mazoezi, tunajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu, tutacheza na Kagera Sugar hapa hapa," alisema Massanza.

Alisema katika mchezo huo, Singida Black Stars itaanza kuwatumia wachezaji wao wapya endapo kocha ataona inafaa kwa sababu wamekamilisha kila kitu, ikiwamo vibali na leseni.

"Niwaambie tu mashabiki wa Singida  wachezaji wetu wote waliosajiliwa kipindi cha dirisha dogo la usajili, wote wapo tayari kucheza, hawana shida ya vibali wala leseni na hata wale Watanzania wenzetu mambo ni shwari, kwa hiyo hakuna kisingizio, wala msiwe na 'stress', waombeeni sana wachezaji wetu maana vita imekuwa kubwa," alisema ofisa huyo.

Nyota wa Singida Black Stars ambao wamepewa uraia wa Tanzania ni pamoja na Josephat Arthur Bada, Emmanuel Keyekeh na Mohammed Domaro Camara.

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ilifanya kikao chake juzi na moja ya mashauri ni mchakato kuhusu nyota hao kupewa uraia wa Tanzania.