Twiga Stars kambini Julai

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 10:54 AM Jun 28 2024
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Clifford Ndimbo.
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Clifford Ndimbo.

TIMU ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), inatarajia kuingia kambini Julai Mosi ili kujiandaa na mechi mbili za kirafiki za kimataifa, imeelezwa.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Clifford Ndimbo, aliliambia gazeti hili jana, Twiga Stars itacheza mechi za kirafiki dhidi ya wenzao wa Tunisia na Botswana.

Ndimbo alisema mechi hizo zinalenga kukiimarisha kikosi hicho ambacho kimekata tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON), ambazo sasa zitafanyika Julai, mwakani nchini Morocco.

"Kikosi cha Twiga Stars kitakuwa na mechi mbili za kirafiki za kimataifa, watacheza dhidi ya Tunisia na Botswana, kitaingia kambini Julai Mosi chini ya Bakari Shime (Kocha Mkuu)," Ndimbo alisema.

Aliwataja wachezaji walioitwa ni Najat Abasi wa JKT, Asha Mrisho (Amani), Lidya Maximilian (JKT), Protasia Mbunda (Fountain Gate), Enekia Kasonga (Eastern Flames), Julietha Singano, Violeth Mwamakamba (Simba), Joyce Lema, Anastazia Katunzi, Janeth Christopher (JKT), Esther Maseke (Bunda) na Diana Lucas kutoka Ame SFK.

Wachezaji wengine ni Aisha Mnunka (Simba), Stumai Athuman, Winifrida Gerald (JKT), Maimuna Kaimu- (ZD ya Misri), Elizabert Charles (Alliance), Aisha Masaka (Bk Hacken), Oppa Clement (Besiktas) na Clara Luvanga wa Al Nasir ya Saudi Arabia.