Waenda kumshuhudia Ronaldo uwanjani

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 07:46 PM Jun 28 2024
Waenda kumshuhudia Ronaldo uwanjani.
Picha: Faustine Feliciane
Waenda kumshuhudia Ronaldo uwanjani.

WAKATI hatua ya 16 bora ya michuano ya Ulaya 'Euro 2024' ikitarajiwa kuanza kesho, baadhi ya mashabiki wa soka wanaondoka nchini leo kwenda Ujerumani kushuhudia michezo ya hatua hiyo ya mtoano.

Kwa sasa katika michezo ya Barani Ulaya, Afrika na Duniani kwa ujumla mashabiki wa soka wanafuatilia michuano hiyo iliyoanza mwanzoni mwa mwezi huu huku timu 16 zikitinga hatua ya mtoano.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mmoja wa mashabiki wanaoenda kushudhudia hatua hiyo, Aileen Tinka, alisema amepata fursa hiyo baada ya kushinda kwenye 'Zigo la Euro' kutoka Tigo.

"Nilishinda na kupewa taarifa, kwa kweli nimefurahi kupata nafasi ya kwenda Ujerumani na kumuona Ronaldo akicheza, siku zote nimekuwa nikimtaza kupitia televisheni lakini naenda kumuona moja kwa moja," alisema Aileen.

Aidha, Meneja Biashara wa kampuni hiyo, Fabian Feliciane, alisema washindi hao wanaondoka nchini leo na mchezo wao wa kwanza kushuhudia kwenye hatua hiyo utakuwa kati ya Ureno dhidi ya Slovania.

"Tayari tumefanya droo ya tano na kupata washindi mbalimbali, washindi wetu wa safari ya Ujerumani wanaondoka kesho (leo) na wale walioshinda fedha na vifaa vya umeme na wenyewe tumewakabidhi zawadi zao," alisema Feliciane.

Mmoja wa washindi wa fedha (shilingi milioni moja), Alex Sanga, alisema amefurahi kupata fedha hizo zitakamzosaidia kwenye mambo mbalimbali.