KIKOSI cha mabingwa wa soka nchini, Yanga leo kitashuka kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa kupimana ubavu na kikosi cha Safari Champion katika mchezo maalum kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Mchezo huo unaosubiriwa na mashabiki mbalimbali umepangwa kuchezwa kuanzia saa 2:15 usiku.
Kikosi kinachokutana na Yanga ni kile ambacho kilipatikana kupitia programu maalum iliyoendeshwa na TBL ambayo ilitafuta vijana wenye vipaji kutoka mikoa mbali mbali na kufanikiwa kuunda timu yenye wachezaji 25.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kocha Mkuu wa timu ya Vijana ya Yanga, Soud Slim anayesimamia kikosi cha Yanga, alisema wamejiandaa vema kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo ambao utakuwa na upinzani mkubwa kutokana na uwezo wachezaji wanaounda kikosi cha Safari Champion.
"Timu ya Safari Champion ni timu yenye ushindani kutokana na aina ya wachezaji waliopo ndani ya kikosi hicho, baadhi nimeona wana uwezo mkubwa sana na wataweza kutoa upinzani kwa kwetu, alisema Slim.
Aidha aliwataka watanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani hapo kushuhudia mchezo huo.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa timu ya Safari Champion, Sekilojo Chambua, alisema amewajenga kisaikolojia wachezaji wake ili waweze kuonyesha viwango vyao katika mchezo huo.
"Nimewajenga kisaikolojia wachezaji wangu kuhakikisha wanafanya vizuri licha ya kuwa hawajawahi kucheza michezo ya usiku," alisema Chambua.
Alisema maandalizi ya siku 26 aliyoyafanya anaamini yatawasaidia kwa kiasi kikubwa kuonyesha vipaji vyao kupitia mchezo huo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED