WAKATI inatarajia kuwakaribisha Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, benchi la ufundi la Yanga limesema wana michezo 15 ya 'ulazima wa kushinda' ili kuhakikisha wanatetea ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.
Ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi inaonyesha mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 10:00 jioni.
Katika msimamo wa ligi hiyo, Yanga yenye pointi 39 iko kwenye nafasi ya pili, nyuma ya vinara, Simba yenye pointi 40, Azam FC inafuatia ikiwa na pointi 36 huku Kagera Sugar yenye pointi 11 iko nafasi ya pili kutoka mkiani.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Mkuu wa Yanga, Saed Ramovic, amesema kwa kuanzia wanataka kupata ushindi katika mchezo wa leo ili kujiongezea hamasa ya kufikia malengo.
Ramovic alisema wameingia katika mzunguko wa pili ambao wanaamini hautakuwa mwepesi kwa sababu kila timu itataka kupambana kupata ushindi ili kufahamu nafasi watakayomaliza baada ya msimu kumalizika.
"Tunakutana na Kagera Sugar... nafahamu na wao wamekuja kujaribu kupata ushindi, hautakuwa mchezo mwepesi lakini ni lazima tupate ushindi, tuna michezo 15 ya mzunguko wa pili, malengo yetu ni kushinda yote, tunataka kuutetea ubingwa wetu," alisema Ramovic.
Kocha huyo alisema pia kuelekea mchezo huo, wachezaji wake wote wapo katika morali kubwa na wanafahamu umuhimu wa kupata pointi tatu.
"Tukipoteza mchezo huu utaanza kutuweka katika wakati mgumu, mzunguko huu wa pili si wa kupoteza ovyo mechi, ni mzunguko ambao ukifanya makosa wenzako watayatumia vizuri ili kusonga mbele," Ramovic alisema.
Naye Ofisa Habari wa timu hiyo, Ali Kamwe, alisema kikosi chao kiko tayari kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki na wanachama wao.
Kamwe amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kuwashangilia wachezaji wao ili wakamilishe kile wanachotarajia kukipata katika mechi hiyo.
"Njooni kwa wingi katika mechi ya kesho (leo), tunaenda kuanza rasmi safari yetu ya kutetea ubingwa, hatutaki kufanya makosa, tumerejea katika mashindano yetu, huku sisi ndio bora zaidi," Kamwe alitamba.
Wakati huo huo, mabosi wa Kagera Sugar, wamesema wamekuja Dar es Salaam kufuata pointi tatu na hawataingia uwanjani kinyonge.
Mtendaji Mkuu wa Kagera Sugar, Thabit Kandoro, alisema wamejiandaa vizuri kwa mchezo huo na hawana 'ugeni' na uwanja wa KMC ambao utakaotumika leo.
"Hatutaingia kinyonge, tunawaheshimu Yanga kama moja ya timu kubwa, lakini ndani ya uwanja tutakuwa sawa," alisema Kandoro.
Aidha, kocha wa timu hiyo, Melis Medo, amesema wamejiandaa vyema kuelekea mechi hiyo na ameandaa mfumo ambao unaweza ukawapa matokeo mazuri.
Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea tena kesho kwa Tabora United kuikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani, Tabora.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED