ACT Wazalendo yamshangaa Wasira kuipotosha safari yao

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 05:12 PM Mar 16 2025
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman
Picha: Mtandao
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman

CHAMA cha ACT Wazalendo, kimesema kimeshangazwa na kauli aliyoitoa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira kwamba kuzuiliwa kwao kuingia Angola, kumetokana wao kutofuata taratibu za kusafiri.

Aidha, kimeitaka serikali kutoka hadharani kueleza kilichotokea wao kuzuiliwa kuingia katika nchi hiyo, ilihali walifuata taratibu zote.

Hayo yamesemwa jana, jijini Dar es Salaam na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman, alipokuwa akielezea kukerwa na baadhi ya viongozi wa CCM waandamizi kupotosha umma kuhusu kilicho watokea.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira
Alisema siku chache zilizopita, Wasira alisema kuzuiliwa kwake kumetokana na yeye kutofuata utaratibu anapotoaka kusafiri kwenda nje ya nchi.

Machi 14 mwaka huu, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasiara akiwa ziarani Wilayani Mbozi Mkoani Songwe alitoa kauli ambayo imetafsiriwa na chama hicho kwamba hawakufuata utaratibu wa kusafiri kwenda nje ya nchi.

Wasira alisema: “Leo nimesoma walikuwa wanaenda Angola sijui wamewanyang’anya ‘passport’ huko ni Angola sio hapa Tanzania hatujawanyang’anya.

“Hata kama ikiwa ‘paasport’ imekwisha muda wake sisi tunawapa labda kama wanajambo lao wametiliwa shaka sisi tungejuaje kuambia tu wasiingie si warudi nyumbani,” alisema Wasira.