ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje ya Nchi, John Mrema ambaye anaongoza kundi la watiania 55 maarufu kama G55, amesena ikipigwa kura ya siri ndani ya CHADEMA wengi watataka chama kiende kwenye uchaguzi.
Akizungunza na waandishi wa habari leo, Dar es Salaam, Aprili 6, 2025, kwa lengo la kufafanua vizuri kwa nini G55, wanaona ni muhimu chama hicho kikashiriki uchaguzi kuliko kususia amesema;
"Nina hakika ikipigwa kura ya siri watu wengi wanaunga mkono tushiriki Uchaguzi Mkuu mwaka huu, kuliko kutokushiriki kwa sababu hawaoni miujiza ya kuweza kuzuia uchaguzi.
Kundi hilo la watiania G55, limesema wanaona dalili za wazi za kuhukumiwa bila kusikilizwa hoja za msingi walizonazo.
"Viongozi watuambie Maria Sarungi ana 'share' (hisa) ngapi katika CHADEMA mpaka anahoji mambo ya chama hiki, hajawahi kusema yeye ni chama gani lakini tunafahamu yeye ni CCM, anaonekana kana kwamba yupo juu hata ya maamuzi ya chama," amesema.
"Mheshimiwa Godbless Lema alitamka kwamba wasiotaka 'No reforms, No election', waondoke CHADEMA, kwahiyo tunaona dalili za kuhukumiwa kabla ya kusikilizwa.
"Sisi kundi la G55, tunaunga mkono madai ya 'reforms' katika mifumo ya uchaguzi na tupo tayari kuongeza jitihada na kuwekeza kupigania mabadiliko ya kimfumo na kisheria, lakini tunasita kuamini katika mpango wa chama kuzuia uchaguzi wa mwaka 2025, njia ya 'No election' hatuoni kama itatufikisha kule tunakotaka kufika," amesema Mrema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED