Malori 100 yakwama mpaka wa Sirari

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:21 PM May 18 2025
Malori
Picha: Samson Chacha
Malori

ZAIDI ya malori 100 yenye shehena za mahindi yamekwama katika mpaka wa Sirari pamoja na kituo cha forodha eneo hilo, mkoani Manyara, kwa kile kinachodaiwa kuwa hayana vibali vya kusafirisha mazao kwenda nje.

Kwa mujibu wa Ofisa Kilimo Kituo cha Forodha Sirari, Phillipo Losotola, malori ya wafanyabiashara yaliyokwama katika kituo hicho cha forodha na mpakani, hayana vibali vya kusafirisha mazao nje ya nchi.

Losotola amesema licha ya malori hayo kuzuiliwa, bado kuna wengine wasio waaminifu wanapita njia za panya usiku, hali inayosababisha kukosekana kwa takwimu sahihi, mbali na elimu kutolewa kwa wafanyabiashara hao.

Baadhi ya wafanyabiashara wa mazao hayo, akiwamo Mabula John, amesema kuwa wanasubiri wenzao wenye vibali kuvusha mahindi yao, huku akitaja tatizo kubwa kuwa ni vitendo vya baadhi yao kukwepa ushuru na kodi na kupita njia za panya.

“Changamoto tunayopata tunaofuata utaratibu kuleta malori hapa TRA ni wenzetu ambao sio waaminifu wao hupita njia za panya bila kulipa kodi wala ushuru wowote na wamechangia bei ya gunia la mahindi kushuka Isebania Kenya kutoka Sh. 105,000 hadi 95,000,” amesema Joseph Mwita.

Mkuu wa Wilaya Tarime, Meja Edward Gowele, wiki iliyopita alitoa onyo kwa wafanyabiashara wanaofanya magendo, wakiwamo wanavusha shehena za mahindi kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Gowele amesema watakamatwa wot watakao vusha mahindi bila kufuata utaratibu kuwa na vibali na leseni, lakini mpaka sasa agizo hilo haijatekelezwa kutokana na hali hiyo kuendelea kuwapo.