WAZIRI wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba ametembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania, ziizopo Kampala nchini Uganda na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini humo, Meja Jenerali Paul Simuli
Nchemba, alifika katika ubalozi huo, baada ya kuhitimisha Mkutano wa 50 wa Benki ya Maendeleo Afrika Mashariki (EADB) na kumpongeza balozi huyo na watumishi wa Ubalozi kwa kazi nzuri wanayofanya.
Katika taarifa iliyotolewa kupitia ukurasa rasmi wa X wa wizara hiyo, Machi 15, 2025 ilieleza kwamba Nchemba, lisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi baina ya mataifa hayo mawili.
Alisema wananchi wa pande zote wanapaswa kuzitumia fursa mbalimbali za ukuzaji biashara kwa manufaa ya nchi hizo mbili, ikizingatiwa kuwa Tanzania na Uganda ni nchi rafiki na zina historia kubwa na ya kujivunia.
Katika ziara hiyo, Nchemba aliambatana na Kamishna wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, DktCharles Mwamwaja na maofisa wengine wa serikali.
Tayari Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB), imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati yake na Tanzania kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED