MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imeendelea kutekeleza programu mbalimbali zinazolenga kufungamanisha sekta ya mafuta na gesi asilia na sekta ya elimu nchini.
Miongoni mwa programu hizo ni pamoja na kutoa fursa kwa wadau wa sekta ya elimu kutembelea miundombinu ya uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia iliyopo katika mikoa inayozalisha gesi asilia nchini kwa lengo la kuongeza uelewa wa wadau hao muhimu.
Katika hilo, Machi 14 mwaka huu, PURA iliwezesha ziara ya wadau kutoka vyuo vya elimu ya juu, vyuo vya elimu ya kati na vyuo vya ufundi nchini kutembelea mitambo ya kuzalisha na kuchakata gesi asilia iliyopo Mkoani Mtwara.
Ziara hiyo pia ilihusisha wadau kutoka mamlaka zinazohusika na udhibiti wa ubora wa elimu ikiwamo Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).
Kupitia ziara hiyo, wadau hao walipata fursa ya kutembelea mitambo ya kuzalisha na kuchakata gesi asilia iliyopo Mnazi Bay inayoendeshwa na kampuni ya Maurel et Prom na mitambo ya kuchakata gesi asilia iliyopo eneo la Madimba inayoendeshwa na GASCO ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Pamoja na maeneo hayo, wadau hao walipata fursa ya kutembelea Chuo cha Ualimu Mtwara (Kawaida) kwa lengo la kuona namna ambavyo matumizi ya gesi asilia yameleta mapinduzi katika chuo hicho baada ya kuacha matumizi ya kuni kama chanzo cha nishati wakati wa kupika na kuhamia katika matumizi ya gesi asilia.
Wakizungumza wakati wa ziara hiyo, wawakilishi wa wadau hao akiwemo Dk. Malehe Setta ambaye ni Mthibiti Ubora Mkuu kutoka TCU,. John Ndega ambaye ni Meneja anayehusika na utafiti ndani ya VETA na Dk Adela Syikilili ambaye ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walisema ziara hiyo, pamoja na kuongeza uelewa, imewasaidia kupata picha halisi ya kiwango cha utaalamu kinachohitajika katika tasnia ya mafuta na gesi asilia.
Mwakilishi kutoka PURA, Musa Ryoba alisema kuwa ziara hiyo ni mwendelezo wa jitihada za Mamlaka hiyo katika kuhakikisha kuwa sekta ya mafuta na gesi asilia nchini inafungamanishwa na sekta nyingine za kiuchumi ikiwamo elimu, kwa kuwa ili sekta ya mafuta na gesi iwe na mchango mkubwa katika uchumi ni lazima ifungamanishwe na sekta nyingine hususan sekta za kimkakati.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED