KIKAO cha Kamati cha Ushauri Mkoa wa Shinyanga (RCC), kimeridhia mapendekezo ya Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kuligawa Jimbo la Solwa, kuwa na majimbo mawili ya uchaguzi ambayo ni Solwa na Itwangi.
Kikao hicho kimefanyika, Machi 15, 2025, kikiongozwa na Mwenyekiti wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha.
Macha, amesema baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kutoa vigezo na mapendekezo kwa ajili ya kuligawa Jimbo la Solwa, kwamba kunapaswa kufuatwa taratibu zingine za vikao, kikiwamo Kikao cha Baraza cha Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kikao cha Kamati cha Ushauri Wilaya ya Shinyanga DCC na kikao cha Mkoa RCC, kupitisha mapendezo ya kuligawa jimbo hilo.
“Kigezo cha kwamba kilichotolewa na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ni Idadi ya watu, kwa mujibu wa sense ya watu na makazi mwaka 2022, jimbo hilo la Solwa lina watu 468,611, lakini takwimu za mwaka huu 2025, kuna ongezeko la watu 503,167, na ukigawanya jimbo la Solwa litakuwa na watu 309,821, na Itwangi 193,346, hivyo tumekidhi vigezo,” amesema Macha.“Kigezo kingine ni ukubwa wa eneo, Jimbo la Solwa lina ukubwa Kilomita za Mraba 4,212, eneo ambalo ni kubwa na lina kigezo jimbo hili kugawanywa,” ameongeza Macha.
Amesema baada ya kikao hicho cha RCC kupitisha na kuridhia mapendekezo ya kuligawa Jimbo hilo la Solwa, taarifa zake zitapelekwa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kabla ya tarehe Machi 26, mwaka huu.
Aidha, INEC, ilitangaza baadhi ya majimbo kugawanywa, na kuwa na majimbo mawili ya uchaguzi, likiwamo Jimbo la Solwa wilayani Shinyanga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED