LICHA ya Juhudi za serikali kuhusu haki za wanawake, suala la ukatili dhidi ya wanawake limeongezeka na kuchukuliwa kama janga.
Akizungumza Machi 21, 2025, kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, wakati wa washilisho la Uchambuzi wa Mwelekeo wa Takwimu kwa maeneo matatu muhimu kutoka kwa Mpango wa Hatua wa Beijing;
Mtaalam wa Jinsia, Leticia Mkurasi, amesema Tanzania inashika nafasi ya 12 kati ya nchi zenye kiwango kikubwa cha ueneaji wa ukatili dhidi ya wanawake katika kanda ya Afrika.
Leticia amesema ukatili unaoripotiwa zaidi ni wa kimwili, kisaikolojia, kingono na kiuchumi na kwamba unazidi kuongezeka na kutokea katika mikoa mingi.
Ameongeza kuwa, kuanzia mwaka 2019 hadi 2021, kuliripotiwa matukio 79 ya mauaji ya wapenzi (IPV), wengi wao walichochewa na wivu.
Akirejea ripoti ya 2023 kutoka kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), amesema inaonesha kuwa kati ya Januari na Septemba 2022, wanawake 472 waliuawa, sawa na wastani wa wanawake 53 kwa kila mwezi.
Pia, ripoti hiyo ilionyesha kuwa mwaka 2018, wanawake 544 waliuawa, mwaka 2019 walikuwa 437, mwaka 2020 walikuwa 431 na mwaka 2024 walikuwa 554.
Shamim Khan, ambaye alichaguliwa kuwa Mbunge wa Morogoro Mjini mwaka 1985, amesema uongozi ni chuo, hivyo ni muhimu watu kuhitimu, ili wengine wapate fursa, akiunga mkono kauli za viongozi kwamba ukomo wa wabunge na madiwani wa viti maalum uwe ni miaka 10.
"Najivunia kuwa mwanamke wa kwanza nchini ambaye nilithubutu na kugombea ubunge na kushinda na baadaye kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Uwekezaji na Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Pia, nilianzisha mfumo wa wanawake kuwa na mabanda yao kwenye maonyesho ya Nane Nane," amesema Shamim.
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, amesema maadhimisho ya mwaka 2025, yanasherehekea utekelezaji wa Mpango Kazi wa Beijing baada ya miaka 30, huku akibainisha changamoto zinazowakabili wanawake na mikakati ya kuendeleza usawa wa jinsia na haki za wanawake.
"Hakika hatua kubwa imepigwa katika kupigania haki za wanawake na usawa, lakini bado kuna kazi kubwa mbele. Vituo vya taarifa na maarifa na serikali vinapaswa kuendelea kuhakikisha wanawake wanapata ulinzi na haki zao," amesema Lilian.
"Uwapo wa bajeti zinazozingatia mlengo wa kijinsia ni hatua muhimu. Mikakati inayotekelezwa ina lengo la kuhakikisha usawa wa kijinsia unakuzwa," ameongeza Hodan.
Mratibu wa Agha Khan Foundation, Nelson Mhando, amesisitiza kuwa miradi ya shirika hilo inajikita katika masuala ya usawa wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na afya na elimu.
Mtaalamu wa masuala ya Jinsia kutoka Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), Clara Maliwa, amesema wanazidi kuondoa vikwazo vinavyowakabili wanawake katika kupigania usawa wa kijinsia, kuhakikisha uhuru na ushiriki wao katika jamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED