KATI ya Januari hadi Julai mwaka huu, ajira 607,475 zimezalishwa nchini ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kufikia lengo la kuzalisha ajira milioni nane lililomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya 2020-2025.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi aliyasema hayo bungeni jana alipojibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Esther Maleko aliyetaka kujua serikali inatumia mbinu gani kuhakikisha watanzania wengi wanapata ajira nje ya nchi na juhudi zinazofanywa kufikia lengo la ilani la upatikanaji ajira milioni nane.
Akijibu swali hilo, Katambi alisema lengo la serikali ni kutoa ajira milioni 1.2 kila mwaka.
"Njia ya pili inahusisha kutumia balozi zetu kutafuta nafasi za kazi kwa watanzania kwenye maeneo hayo. Tatu, wanadiaspora wa Tanzania pia ni sehemu ya mkakati wetu wa kupata fursa za ajira kwa watanzania," alisema.
Katambi alisema watanzania pia wanapata ajira nje ya nchi kwa juhudi binafsi kulingana na sifa zao za kielimu au vigezo vingine kama vile kuwa wanamichezo au kuwa na vipaji mbalimbali.
"Njia nyingine ni kupitia taasisi za elimu, wizara na vyuo vikuu ambako baadhi ya watanzania wanapata ajira nje ya nchi, zikiwamo nafasi za utafiti na fursa kupitia mashirika ya Umoja wa Mataifa. Kwa mfano, Dk. Faustine Ndugulile," Naibu Waziri alisema.
Katambi pia alisema serikali itafanya Utafiti Jumuishi wa Nguvu Kazi (ILFS) na Utafiti wa Mapato ya Ajira kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Benki ya Dunia.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Grace Tendega, alihoji kuhusu mkakati wa serikali kubaini fursa za ajira nje ya nchi na kuzifikisha kwa watanzania.
Akijibu swali hilo, Katambi alisema serikali tayari imeanza kutekeleza mpango maalumu kupitia Kitengo cha Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) ili kubaini ajira zinazotangazwa mtandaoni na kuwafikia watanzania katika kanzidata, hata kuwasaidia kwa mafunzo ili kuhakikisha wanastahili kupata ajira hizo.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Shally Raymond alihoji wahitimu wangapi wa vyuo wanafanya kazi ya kujitolea na wangapi wameajiriwa na kujiajiri baada ya kujitolea.
Naibu Waziri Katambi alisema serikali ilianza rasmi kuratibu utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Mafunzo ya Uzoefu wa Kazi kwa Wahitimu mwaka 2019/20 na tangu kuanza utekelezaji programu hiyo, wahitimu 21,280 wamenufaika. Kati yao, wanaume ni 11,281 na wanawake ni 9,999.
Alisema miongoni mwa wanufaika hao, 3,772 wamepata kazi, wanaume wakiwa ni 2,265 na wanawake 1,507.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED