WIZARA ya Viwanda na Biashara imewataka wafanyabiashara na wauzaji vyakula nchini kuacha kuweka vyakula juani wanapoviuza ili kuwaepusha walaji dhidi ya sumu.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, ambaye yuko katika ziara ya siku tatu mkoani Singida, alitoa agizo hilo jana baada ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kula ya alizeti cha Singida Fresh Oil Mill kilichoko Manispaa ya Singida.
“Wauzaji na ndugu zangu wafanyabiashara muuze vyakula kwenye mazingira sahihi, si kwenye jua. Si tu mafuta ya kula hata vyakula vingine vitunze vizuri ili hata mlaji asile sumu,” alisema.
Kigahe alisema wazalishaji lazima watambue kuwa wanaingia kwenye biashara ya ushindani ambayo mafuta wanayozalisha hawauzi tu hapa nchini, bali hata nje ya nchi, hivyo lazima bidhaa zizalishwe kwa ubora.
“Wapo watu wachache wasiokuwa waaminifu wanaweza kutumia nembo na kuweka mafuta yasiyofaa halafu akapeleka nje, ikaonekana mafuta yanayotoka Tanzania hayako vizuri, tuwe makini na hili,” alitoa tahadhari.
Akizungumza baada ya kupewa taarifa ya mkoa, Naibu Waziri Kigahe alisema wizara itahakikisha inaweka mikakati ya kusaidia mkoa wa Singida ili ufikie malengo ya kuzalisha mafuta ya kupikia ya alizeti yatayotosheleza kulisha nchi na mengine kuuzwa nje ya nchi. Alisema mahitaji ya mafuta ya kupikia ya alizeti ni makubwa nchini, hivyo mkoa wa Singida uweke kipaumbele namba moja cha kuzalisha mafuta ya alizeti.
“Hii iwe fursa namba moja kwa Singida kusimama kama mkoa unaoweza kuzalisha mafuta ya alizeti kulisha nchi na kuuza nje, soko lipo kubwa la ndani na nje, hata kwa jirani zetu DRC ( Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) pamoja na changamoto waliyonayo,” alisema.
Naibu Waziri Kihage alisema mkakati wa serikali ni kutaka kuona Singida inakuwa mkoa wa kimkakati wa viwanda ambao wazalishaji wadogo wa mafuta watakuwa wanazalisha na kuwauzia wenye viwanda vikubwa ili mafuta yaongezwe thamani yafae kiafya.
Alisema kutakapowekwa utaratibu kwa wazalisha wadogo kuuza mafuta wanayozalisha kwa wenye viwanda vikubwa, mbali na kuwa na uhakika wa soko, uzalishaji mafuta yenye ubora pia utaongezeka nchini. Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego alisema mkoa umetenga hekta 6,000 kwa ajili ya kuwekeza kwenye viwanda ili kufanya mkoa kuwa na viwanda vingi vitakavyosaidia kuinua uchumi wa mkoa.
Dendego alishukuru Bunge kwa kuweka utaratibu mzuri ambao utalinda mafuta yanayozalishwa nchini kwa kuwa na uhakika wa soko kwa wazalishaji bidhaa hiyo.
Alisema wafanyabiashara wa mkoa wa Singida wamekuwa na ushirikiano mzuri kwa serikali, wakilipa kodi kama taratibu na sheria zinavyoelekeza na hivyo kufanya Singida kuwa miongoni mwa mikoa ambayo inafanya vizuri katika ukusanyaji mapato.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED