KITUO Cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), kimeandaa mafunzo kwa ajili ya kuibua miradi inayoweza kutekelezwa kwa utaratibu wa ubia katika mikoa 12 yatakayohusisha makundi mbalimbali.
Kwa mujibu wa umma iliyotolewa na PPPC, jukumu hilo la kuibua miradi litafanyika kwa siku 28 na litahusisha wataalam wakiwemo wahadhari kutoka vyuo vikuu, TAMISEMI na PPP Center ambao watashiriki moja kwa moja kuibua miradi katika mikoa hiyo.
Taarifa hiyo iliitaja mikoa hiyo kuwa ni Pwani, Mtwara, Morogoro, Tanga, Simiyu, Kilimanjaro, Mbeya, Songwe, Mwanza, Kigoma, Dodoma na Arusha pamoja na halmashauri zake.
“Lengo ni kutengeneza orodha ya miradi (PPP Project Pipeline) ambayo itafanikisha maendeleo endelevu kwa kushirikiana na sekta binafsi,”alisema.
Aidha, zoezi hilo litahusisha kutoa mafunzo kuhusu dhana ya PPP kwa sekretarieti za mikoa na halmashauri zake; kuibua miradi yenye sifa ya kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP; kuandaa maandiko kwa miradi itakayopendekezwa na halmshauri husika.
Pia kuandaa matangazo ya miradi iliyopendekezwa kwa ajili ya kupata wawekezaji watakaotekeleza miradi hiyo; na kuweka miradi iliyopendekezwa katika ramani za Halmashauri kwa kutumia teknolojia ya GIS.
“Katika hatua hii, serikali inatarajia kuimarisha mazingira ya uwekezaji kwa kushirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha huduma kwa wananchi,”alisema.
Kisheria PPPC imepewa jukumu la kutoa usaidizi wa kiufundi pamoja na mafunzo kwa Mamlaka za Serikali za Serikali, zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa, katika kuibua, kuandaa na kusimamia utekelezaji wa miradi ya ubia baina ya sekta umma na binafsi (PPP).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED