SERIKALI inaendelea kuangalia namna ya kupunguza au kuondoa kodi nyingine za uagizaji magari yenye mfumo wa gesi ili kuhamasisha matumizi ya gesi asilia.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga aliyasema hayo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Grace Tendega.
Mbunge huyo alitaka kujua mpango wa serikali kupunguza baadhi ya kodi ili watanzania wengi waingize magari yenye mfumo wa nishati ya gesi.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kapinga alisema serikali kupitia bajeti yake ya mwaka 2023/24, ilitoa msamaha wa Kodi ya Ushuru wa Forodha asilimia 25 kwa injini za magari yanayotumia gesi asilia yanapoingizwa nchini.
Alisema serikali pia inaendelea na hatua mbalimbali za kuhamasisha sekta binafsi kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye viwanda vinavyotengeneza vipuri vinavyotumika katika kufunga mfumo wa matumizi ya gesi asilia kwenye magari na mitambo nchini.
Katika swali la nyongeza, mbunge huyo alisema majibu hayo yanaonesha hakuna kiwanda kinachotengeneza vipuri nchini kutoka mfumo wa mafuta kwenda wa gesi na kuhoji wamepatikana wawekezaji wangapi baada ya sekta binafsi kushirikishwa kutengeneze vipuri hivyo.
“Serikali haioni haja ya kupunguza au kuondoa kodi kabisa katika vipuri vinavyoingizwa nchini," mbunge huyo alihoji.
Akijibu maswali hayo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba alisema serikali imechukua hatua ambapo kwa mwaka 2024/25, imezingatia kupunguza kodi kwenye magari na vipuri vinavyotumia gesi.
"Hata hivyo, tumepokea maoni ya mbunge na tutaendelea kuyafanyia kazi hata katika mwaka wa fedha 2025/26 ambao tumeanza maandalizi ya kuandaa hatua za kikodi mpya na msukumo wa serikali ikizingatiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara ya matumizi ya nishati safi," alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Esther Matiko, akiuliza swali la nyongeza, alisema katika kuhamasisha matumizi ya gesi kwenye magari na mzigo mkubwa upo kwenye malori na mabasi na kwamba kuna vituo 14 ambavyo vinabadili magari ya petroli pekee kwenda mfumo wa gesi.
Alihoji mkakati wa serikali kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji kwa kuweka kituo cha kubadili magari ya dizeli.
Naibu Waziri Kapinga, akijibu swali hilo, alikiri kuwa hivi sasa vituo vingi ni vya kubadilisha mfumo wa petroli na kwamba wanaendelea kujenga vituo ili kuwa na cha magari ya dizeli.
Alifafanua kuwa mifumo ina tofauti kubwa na kwa petroli kwenda gesi ni rahisi kuliko yanayotumia dizeli, lakini kwa kushirikiana na sekta binafsi vitawekwa vituo hivyo ili kukidhi mahitaji yaliyopo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED