CHAMA cha ACT Wazalendo, kimeainisha maeneo maeneo muhimu, iwapo serikali na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), kitayatekeleza kwa vitendo, kwa kujenga msingi wa kuaminiana miongoni mwa wadau wa uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Hayo yamebainishwa katika taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hicho, Shangwe Ayo, kwenda kwa vyombo vya habari leo, Aprili 5, 2025.
Katika taarifa hiyo, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, akizungumza katika Kongamano la Tatu la Operesheni Linda Demokrasia, lililofanyika mkoani Kigoma, amesema chama hicho kina hoja sita;
Kwanza, kuhakikisha kuwa wajumbe wa sasa wa INEC, wanaondolewa na wajumbe wapya wanateuliwa kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa kwenye Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, ikiwamo kutangaza nafasi hizo na kufanya usaili kwa Watanzania wenye sifa kupewa nafasi ya kuwa Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi.
Pili, Mchinjita amesema, ni lazima vyombo vya ulinzi na usalama vijiondoe katika kushiriki katika hujuma za kupora uchaguzi, akisema uzoefu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, Uchaguzi Mkuu 2020 na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, umeonesha kuwa vyombo vya dola, ikiwamo Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa, vimejiingiza katika wizi kubariki na kushiriki katika vitendo vya wizi wa kura.
Mchinjita, amesema tatu, ni ACT Wazalendo kusisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri kutokuwa wasimamizi wa Uchaguzi.
Amesema INEC, inapaswa kuhakikisha kuwa mchakato unaoendelea sasa wa uteuzi wa wasimamizi na wasimamizi wa uchaguzi hauwahusishi Wakurugenzi wa Halmashauri, ambao takribani wote ni makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Nne, hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa kuhakikisha kuwa kura feki zinadhibitiwa kwenye mchakato wa uchaguzi.
“Lazima kuwa na uwazi na ushirikishaji kwenye mchakato mzima wa uzalishaji, usambazaji na udhibiti wa karatasi za kupigia kura.
“Tano, mawakala ni lazima wawe huru katika vituo vya kupigia kura. Mchakato mzima wa upatikanaji, uapishaji na uwepo wa mawakala katika vituo vya kupigia kura ni lazima uzingatie maslahi mapana ya wagombea ikiwemo mawakala kupatiwa nakala za matokeo. Pia iwe ni mwiko kwa mawakala kuondolewa kwenye vituo vya kupigia kura.”
Suala la sita, amesema kusiwe na kuenguliwa kwa wagombea na INEC iweke utaratibu wa kurekebishwa kwa makosa ya kiuandishi katika fomu za wagombea badala ya kuendelea kuwaengua wagombea wa upinzani pekee.
Kwa upande wa Zanzibar, Mchinjita amesema kuwa masuala ya kipaumbele ni kuondolewa kwa kura ya mapema, kuondolewa kwa Mkurugenzi wa ZEC na Sekretarieti yake na uandikishaji wa wapigakura bila ubaguzi.
Mchinjita ameweka bayana kuwa hoja hizi zitawasilishwa majadiliano yanayoendelea kupitia Kituo cha Demokrasia (TCD) na msimamo wa Chama hicho wa kutaka Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 ufutwe na ufanywe sambamba na Uchaguzi Mkuu 2025.
Mchinjita ameweka bayana kuwa Operesheni Linda Demokrasia, ina lengo la kurejesha thamani ya kura ya kila Mtanzania na kwamba ACT Wazalendo inaendelea kuwahamasisha wananchi kuwa tayari kupigania thamani ya kura.
ACT-Wazalendo, inaendelea na Makongamano ya viongozi wa ngazi za chini kufafanua msimamo wa Chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.
Kongamano la Mkoa wa Kigoma ni la tatu, likitanguliwa na makongamano ya mikoa ya Dar es Salaam na Lindi.
Baada ya Kigoma, ACT Wazalendo kinatarajiwa kufanya Kongamano la nne katika mkoa wa Songwe Aprili 12, 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED