Rais Samia aondoa viza kwa watalii wa Angola, akaribisha wawekezaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:58 PM Apr 08 2025

Rais  Samia Suluhu Hassan.
Picha: Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia Suluhu Hassan, ametangaza kuondoa viza kwa watalii kutoka Angola wanaokuja nchini, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.

Aidha, amewakaribisha wafanyabiashara wa Angola kutembelea Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kujionea fursa mbalimbali zilizopo, hususan katika sekta ya madini, ambazo pia zinatarajiwa kuchangia katika utoaji wa ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Rais Samia alibainisha hayo wakati akizingumza na waandishi wa habari wakati akiwa katika ziara ya siku tatu Luanda, nchini Angola. Amesema kuwa mbali na madini, kuna fursa lukuki katika sekta ya kilimo, utalii na uchumi wa buluu ambazo wawekezaji kutoka Angola wanaweza kuzifanyia kazi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Katika hatua nyingine, Rais Samia alimwalika Rais wa Angola, João Manuel Lourenço, kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yatakayofanyika mwezi Julai, mwaka huu.

1

Ampigia bede Prof. Janabi

Ameliomba Taifa la Angola kuiunga mkono Tanzania kwenye nafasi inayogombaniwa ya Ukurugenzi kwenye Shirika la Afya Duniani (WHO), ambayo Tanzania inawakilishwa mgombea wake Profesa Mohamed Janabi.

Akizumgumza katika mkutano huo, Rais wa Angola, Joao Manual Lorenco, alisema anaishukuru Tanzania kwa kujitoa kuisidia nchi yao ilipokuwa kwenye harakati za ukombozi kwa kuwafadhili raia wake kwa kuwapa makazi, mahitaji mengine na usalama.

Alisema historia iliyowekwa na Hayati Nyerere kwenye nchi yao, imewafanya kumpa heshima ya kumpa jina la hospitali kubwa nchini humo itakayozinduliwa mwezi Novemba, mwaka huu wakati nchi hiyo inaposherehekea miaka 50 ya uhuru wake na wamempa heshima Rais Samia kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wake.

Aidha, ameahidi kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili na bara zima la Afrika.

Awali, katika ziara hiyo Rais Samia alitembelea mnara wa Mashujaa wa Angola na kuweka shada la maua na alihutubia Bunge la nchi hiyo akiwa Rais wa kwanza mwanamke kulihutibia.

2