MoCU yapewa mchongo kuanzisha Kituo Atamizi cha Ubunifu

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 02:56 PM May 17 2025
Mfanyabiashara na mmilili wa kampuni za Izack Enterprises akizungumza na wabunifu katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi jana.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mfanyabiashara na mmilili wa kampuni za Izack Enterprises akizungumza na wabunifu katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi jana.

Mfanyabiashara tajiri mwenye umri mdogo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Izack Ngowi, amekipa ‘darasa’ Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), akikitaka kione uwezekano wa kutafuta fedha, kwa ajili ya kuanzisha Kituo Atamizi cha Ubunifu (Innovation Hub), kitakachosaidia kukuza na kulea vipaji na ubunifu kwa wanafunzi na wafanyakazi wengine nchini.

Amesema Kituo hicho Atamizi cha Ubunifu, licha ya kuwa fursa ya ajira kwa vijana, kitasaidia pamoja na mambo mengine kampuni changa (startups), ili kujenga mazingira mazuri ya ukuaji wa bunifu za watu na kuzilea hadi kuwa kampuni kubwa.

Akizungumza jana chuoni hapo (Mei 16, 2025) katika kilele cha kazi za kibunifu za wanafunzi kwa mwaka 2025, mfanyabiashara huyo, ambaye ni mmiliki wa Kampuni za Izack Enterprises nchini, amesema kituo hicho kitasaidia sana kuwa na mwendelezo wa vipaji na ubunifu mzuri kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.

Mfanyabiashara Izack Enterprises, wa kwanza kulia, akisikiliza maelezo ya mmoja wa wabunifu katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

“Nakipa changamoto, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, kuona uwezekano wa kutafuta na kutengeneza fedha, kwa ajili ya kuanzisha Kituo Atamizi cha Ubunifu (Innovation Hub), kitakachosaidia katika kukuza na kulea vipaji na ubunifu kwa wanafunzi na wafanyakazi wengine.


…Na katika hili la ubunifu wa wanafunzi wa chuo hiki; kampuni yangu inatoa nafasi 10 za ajira kwa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi. Niko na HR wangu hapa (Ofisa Rasilimali Watu) na msaidizi wangu Danny;


Nitahakikisha hii ahadi niliyoitoa tunaikamilisha. Niwashukuru sana MoCU kwa kulea vijana hawa wenye ubunifu. Katika kampuni yetu, tayari tumeajiri wafanyakazi 15 kutoka chuo hiki; ambao ni zao la chuo hiki. Wafanya kazi vizuri katika idara mbalimbali ikiwemo Department ya HRM, masoko, mauzo pamoja na uhasibu.”


Makamu Mkuu wa Chuo hicho cha MoCU (Taaluma), Prof. John Safari, amesema maonyesho hayo ya tisa ya ubunifu wa stadi za kazi kwa wanafunzi, yaani Carrier Fair; amesema zaidi ya wanafunzi 118 kutoka program mbalimbali, wameonyesha huduma na bidhaa mbalimbali walizobuni wenyewe kutokana na utashi walionao; wa kijasiriamali pamoja na ujuzi ambao wameupata darasani.

“Ninampongeza Izack Interprises, kwa kuajiri nguvu kazi ya watu 280. Ni taasisi ambayo inaweza kuhudumia Watanzania wengi. Kwa mfano Izack Ngowi, yeye ana kampuni nyingi, ambazo kwa kweli nasema hakuna mtu anaweza kukusudia haya yote na akawa mtalaam, yaani anashughulika na electronics, usafirishaji, microfinance lakini ana ushirikiano.

Zaidi ameongeza: “Ukijua strength yako ni ipi ifanyie kazi, udhaifu shughulika na watu wengine. Kwa hiyo, ameajiri wataalam wengi sana, anastahili pongezi.”