Waziri Kivuli wa TAMISEMI kupitia ACT-Wazalendo, Kulthumu Mchuchuli, leo Mei 16, 2025, amechukua rasmi fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Rufiji, katika hatua inayotafsiriwa kuwa mwendelezo wa mapambano ya ukombozi wa wananchi dhidi ya mfumo usiowajali.
Fomu hiyo amekabidhiwa na Katibu wa Jimbo, Said Matimbwa, mbele ya umati wa wafuasi wa ACT-Wazalendo na wakazi wa Rufiji waliokusanyika kushuhudia tukio hilo.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu, Mchuchuli amesisitiza kuwa ni wakati wa wananchi wa Rufiji kunufaika moja kwa moja na rasilimali zao, hasa fedha za huduma kwa jamii (CSR) kutoka mradi mkubwa wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
“Haiingii akilini bilioni zaidi ya 260 za CSR zipotee kana kwamba si haki ya wananchi wa Rufiji. Kama nitapewa ridhaa na wananchi, nitahakikisha fedha hizi zinarejea kwa wananchi na kutumika kwa maendeleo ya kweli — shule, zahanati, maji na miundombinu ya maana,” amesema kwa msisitizo.
ACT-Wazalendo kupitia uchambuzi wake wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) 2023/24, ilibainisha kuwa fedha hizo za CSR, ambazo zilipaswa kutolewa tangu mwaka 2019, zimeendelea kuzuiliwa bila sababu za msingi, huku serikali ya CCM ikituhumiwa kwa uzembe na kufumbia macho maslahi ya watu wa Rufiji, Kibiti na maeneo mengine yaliyo jirani na mradi huo.
Kwa kuchukua fomu ya kugombea ubunge, Mchuchuli amejiunga na safu ya viongozi wa ACT-Wazalendo wanaoamini kuwa ushiriki wa kweli katika siasa za uchaguzi ni sehemu ya mapambano dhidi ya mfumo wa kifisadi na ubabe wa CCM.
“Ni wakati wetu. Ni wakati wa Wanarufiji kuamka na kuchukua hatima yao mikononi mwao. Hatuhitaji huruma, tunahitaji haki,” alihitimisha Mchuchuli.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED