Hakuna mwenye hati miliki ya kugombea ACT Wazalendo-Ado

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:34 PM May 16 2025
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu amesema kuwa Chama hicho kinaamini katika kuonesha demokrasia kwa vitendo hivyo hakuna mtu yeyote ambaye ana hatimiliki ya kugombea ndani ya Chama.

Ado amesema hayo kwenye tukio la Songwe Day lililowakutanisha watiania wanaogombea nafasi za Ubunge na Udiwani kutoka Majimbo yote ya Mkoa wa Songwe jana tarehe 15 Mei 2025. Jumla ya wagombea nane wa ubunge wamechukua fomu Mkoani Songwe hadi sasa ambao ni Peter Kayuni (Vwawa), Michael Nyilawila (Songwe), Himid Siwale (Momba) na Ezekia Zambi, Nestory Tweneshe, Viniwa Arusha, Emanuel Kalinga (Mbozi).


Ado amesema kuwa kwa mujibu wa taratibu za Chama cha ACT Wazalendo wanachama wote wana haki sawa katika kugombea nafasi yoyote kwenye Uchaguzi Mkuu 2025.


"Sisi tunaamini kuwa kama unahubiri demokrasia unapaswa kuionesha ndani ya Chama kabla ya kwenda kuipigania njia ya Chama. Kwenye Chama chetu, kwa nafasi zote za Urais, ubunge, ubunge Viti Maalum, Udiwani na Udiwani Viti Maalum kila mwanachama mwenye sifa ana haki ya kugombea" alisema Ado.



"Kiongozi wa Chama Ndugu Dorothy Semu amegombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyekiti wa Chama Ndugu Othman Masoud Urais wa Zanzibar, Makamu Mwenyekiti Bara Ndugu Isihaka Mchinjita Ubunge wa Lindi, Kiongozi wa Chama Mstaafu Ndugu Zitto Kabwe Ubunge wa Kigoma Mjini, Mimi Katibu Mkuu Ubunge wa Tunduru Kaskazini lakini sote tunapenda na tupo tayari kwa ushindani. Anayetaka kuchukua fomu dhidi ya yeyote kati yetu milango ipo wazi. Sisi ACT Wazalendo hatuna utaratibu wa fomu moja kwa lazima kama CCM" alisisitiza Ado.


Kwa msisitizo Ado amesema kuwa Ofisi yake inatoa onyo kwa Katibu yeyote wa Kata au Jimbo ambaye ataweka vikwazo kwa mgombea yeyote kuchukua fomu akisisitiza kuwa hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.

Katika hatua nyingine Ado amesema kuwa Chama hicho kinaendelea na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2025 sambamba na kupigania mageuzi ya msingi katika mfumo wa uchaguzi.

 Amesema maeneo ambayo wanayapigania ni sita ambayo ni; mosi, Wakurugenzi wa Halmashauri wasisimamie uchaguzi, pili wajumbe wapya wa Tume ya Uchaguzi wateuliwe kwa utaratibu uliowekwa kwenye sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, tatu kusiwe na kura feki, nne wagombea wasienguliwe hovyo, tano vyombo vya ulinzi na usalama visishiriki hujuma kwenye uchaguzi na sita mawakala wa vyama wasibugudhiwe, wawe huru vituoni.

Leo tarehe 16 Mei 2025, Ado atakuwa mgeni rasmi wa tukio la Mbeya Day litalowakutanisha watiania wa Ubunge na Udiwani kutoka majimbo yote ya Mkoa wa Mbeya.