Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana, amesema serikali kwa sasa ipo katika mkakati wa kukuza utalii wa vyakula kwa kuwa kila kabila lina vyakula vyake na hivyo itakuwa rahisi kushawishi watalii kuja kuviona.
Waziri huyo ameyasema hayo leo katika mahafali ya vijana 100 waliohitimu katika Fani ya Utalii na Ukarimu katika Chuo Cha Taifa Cha Utalii (NCT) kwa ufadhili wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL).
Dk Pindi amesema lengo la kuja na utalii wa vyakula ni kuvutia zaidi watalii nchini na kuongeza pato la taifa kwa kuwa vyakula vingi vinavyopatikana kwetu kwao havipo. Aidha amekumbushia kuwa filamu ya 'Royal Tour' imeongeza mamilioni ya watalii nchini na kwamba juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan zimezaa matunda.
"Kwa Sasa tuna zaidi ya watalii 5,000,000 wanaokuja nchini suala hilii limewezekana kutokana na nchi yetu kuwa na amani pamoja na mazingira wezeshi kwa watalii kuja nchini. Aidha aliwataka SBL kuwaunganisha wahitimu hao na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma za kitalii na ukarimu ili waweze kunufaika na elimu waliyoipata.
"Nimefurahi kuona SBL wamefadhiri vijana zaidi ya 100 kwaajili ya kuwapa mafunzo ya kutoa huduma bora. Mtalii anapokuja nchini anahitaji huduma bora na chakula kizuri kupitia wahitimu hawa watakwenda kutusaidia vizuri katika eneo hilo" amesema huku akishangiliwa na wahitimu hao na kusisitiza ni wajibu wake kuwatafutia sehemuza kufanya kazi
Aidha amewataka SBL kuchukua na vijana kutoka mikoa mingine ili kutanua zaidi elimu hiyo. Awali Mkuu wa Wilaya, Ilala Edward Mpogoro aliwashukuru SBL kwa kufadhili wanafunzi Katika masuala ya utalii akisifu wamechagua jambo sahihi.
"Serengeti wangeweza kutumia fedha zao kutangza bia zao lakini wameamua kufadhiri mafunzo ya miezi minne kwaajili ya kuwapa vijana elimu hili ni jambo kubwa sana" amesema Mpogoro
Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma SBL, John Wanyancha, aliwashukuru wahitimu hao akisifu wamekuwa sehemu ya familia ya kampuni hiyo na wapo tayari kuendelea kuwaunga mkono ili elimu waliyoipata iweze kuwafikisha mbali. Amesema programu hiyo ni endelevu na kwa wananfuzni wengine wanakaribishwa mwakani kuomba fursa hizo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED