WAUGUZI wa Manispaa ya Shinyanga, wameadhimisha siku ya Wauguzi Duniani kwa matendo ya huruma kwa wagonjwa katika Manispaa hiyo, ikiwa ni sehemu ya kumuenzi muuguzi wa kwanza duniani Florence Nightingale.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Mei 16, 2025 katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, ambapo wauguzi walitembelea wagonjwa na kuwapatia zawadi mbalimbali zikiwemo sabuni na mafuta.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze, ambaye amewapongeza wauguzi kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhudumia wagonjwa kwa moyo wa huruma, licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Nawapongeza sana wauguzi kwa huduma nzuri mnayotoa. Mimi mwenyewe hivi karibuni nilipopata changamoto ya kiafya nilihudumiwa vizuri katika hospitali hii, na baadhi yenu hamkunijua kabisa lakini mlinitibu kwa upendo sawa na wagonjwa wengine,hii inaonesha kuwa mnatoa huduma bila upendeleo,” amesema Kagunze.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuwaboreshea mazingira mazuri ya utendaji kazi, na ndiyo maana hata ilitoa pesa na kuikarabati Hospitali ya Manispaa hiyo,pamoja na hivi karibuni Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alitangaza nyongeza ya mshahara na kwamba hiyo ni kuwajali watumishi.
Kwa upande wake, Kaimu Muuguzi Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Anna Maganga, amemshukuru Mkurugenzi kwa kuwathamini wauguzi na kutoa fursa ya viwanja,huku akiwataka wauguzi wachangamkie fursa hiyo ya kupata viwanja.
Anna amesema kuwa taaluma ya uuguzi ni sadaka, na kwamba wataendelea kutoa sadaka hiyo kwa uaminifu kama alivyokuwa akifanya muuguzi wa kwanza duniani Florence Nightingale, kwa kuhudumia wagonjwa kwa upendo na moyo mmoja.
Naye Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Frola Kajumla, amesema taaluma ya uuguzi inahitaji kutambuliwa, kuungwa mkono na kuwekewa mazingira mazuri ya kazi ikiwa wauguzi ndiyo wanaokaa muda mwingi na wagonjwa katika kuwahudumia.
Nao baadhi ya wagonjwa ambao wamelazwa katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga akiwamo Matha Mhoja katika Wodi ya wazazi,amewashukuru Wauguzi kwa kuwahudumia vizuri, na kwamba kutokana na huduma bora amejifungua mtoto wake salama akiwa na afya njema.
Ingawa Siku ya Wauguzi Duniani huadhimishwa kila Mei 12, wauguzi wa Manispaa ya Shinyanga wamefanya maadhimisho hayo leo Mei 16, 2025 kwa kumuenzi muasisi wa taaluma ya uuguzi duniani Florence Nightingale.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED