Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita, amekutana na viongozi wa Ngome ya Wazee kutoka kata 20 za Manispaa ya Lindi katika kikao kilicholenga kujadili mwelekeo wa chama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Katika mkutano huo, Makamu Mwenyekiti aliwaeleza wazee hao kuwa chama kimeamua kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo kama sehemu ya utekelezaji wa Operesheni Linda Demokrasia — kampeni ya kulinda haki za kidemokrasia, usawa, na misingi ya utawala bora nchini.
“CCM wajiandae. Mwaka huu hawatakabiliana na upinzani wa maneno bali wa mikakati. Wakati wa kuoneana hofu umeisha. Tunakwenda kwenye uchaguzi tukijua tunapigania mustakabali wa taifa hili,” alisema Mchinjita kwa msisitizo.
Wazee walipokea kwa mikono miwili maamuzi ya chama chao kushiriki uchaguzi, wakisisitiza kuwa historia na uzoefu wao unaonesha wazi kuwa hakuna mafanikio yoyote yanayopatikana bila mapambano. Walikumbushia juhudi walizozifanya katika Uchaguzi wa mwaka 2010, wakisema walishiriki kwa karibu kulinda na kushinikiza matokeo sahihi yatangazwe.
"Hatutakuwa watazamaji. Tumejifunza kuwa mafanikio yoyote hayaji yenyewe, lazima yapiganiwe," walisema baadhi ya wazee walioshiriki mkutano huo.
Mkutano huo ni sehemu ya mwendelezo wa maandalizi ya ACT Wazalendo kuelekea uchaguzi, huku wazee wakiahidi kutoa mchango wao mkubwa katika kuhakikisha demokrasia inalindwa na sauti ya wananchi inasikika na kuheshimiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED