Mfalme Zumaridi aachiwa kwa dhamana

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 02:39 PM May 16 2025
Diana Bundala maarufu kama mfalme Zumaridi
PICHA: MTANDAO
Diana Bundala maarufu kama mfalme Zumaridi

Diana Bundala maarufu kama mfalme Zumaridi aliyetiwa mbaroni na jeshi la polisi jana Mei 15, 2025 kwa kosa la kuendesha shughuli za ibada bila kuwa na kibali ameachiwa kwa dhamana baada ya kukidhi masharti.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza pamoja na kosa hilo, Zumaridi alikuwa anakabiliwa na shtaka la kusababisha kelele kwa majirani akidaiwa kuendesha mahubiri yake kwa sauti ya juu.
Baada ya Jeshi hilo kumkamata alifanyiwa mahojiano katika kituo kikuu cha polisi Nyamagana na hatimaye kudhaminiwa jana baada kukidhi masharti ya dhamana akiwa polisi.Baada ya kupatiwa dhamana Zumaridi alitakiwa kuripoti kituoni hapo leo Mei 16 kwaajili ya taratibu za kisheria.
Kukamatwa kwa Zumaridi na kufunguliwa mashtaka hayo kunakuja baada ya miaka mitatu tangu alipokamatwa mwaka 2022 na jeshi la polisi akikabiliwa na makosa matatu yakiwemo ya kufanya mkusanyiko usio halali, usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na kuwazuia maofisa ustawi wa jamii kutekeleza wajibu wao na kuzuia maafisa wa serikali kutekeleza jukumu lao ambapo alikamatwa yeye na wafuasi wake zaidi ya 80
Aidha Januari 25, 2023 Zumaridi pamoja na wafuasi wake wanne walikutwa na hatia katika makosa ya kuzuia maofisa ustawi wa jamii kutekeleza wajibu wao pamoja na kuwazuia maafisa wa serikali kutekeleza jukumu lao na kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela.
Hata hivyo Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza iliamuru atumikie mwezi mmoja pekee gerezani kutokana na kukaa mahabusu katika gereza kuu la Butimba kwa muda wa miezi kumi na moja.