Serikali imesema katika kipindi cha Julai, 2024 hadi Machi, 2025 jumla ya madereva 7,232 walisajiliwa kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Usafiri Ardhini (RRIMS) na kutahiniwa kupitia Mfumo wa Kutahini Madereva (Drivers Testing System - DTS) ambapo kati ya hao madereva 1,550 walithibitishwa.
Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa amesema hayo jana Mei 15, bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2025/2026. Amesema serikali imeweka utaratibu wa lazima wa madereva wa safari za usiku kwa mabasi ya abiria kuwa na kitufe cha utambuzi (i-Button).Aidha, amesema serikali inaendelea kuboresha mfumo huo ili utumike kuthibitisha madereva wa treni.
Kwa upande wa usajili wa wahudumu amesema hadi kufikia Machi 2025, LATRA ilisajili wahudumu 560 baada ya kupewa mafunzo ambayo yalitolewa kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED