MWALIMU Mkuu wa shule ya msingi Ngilimba iliyopo kata ya Ulowa Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, Erick Ombeni anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma ya kumchapa viboko mwanafunzi wa darasa la saba Julius Paul (15) na kumsababishia majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kwa mujibu wa waraka wa elimu namba 24 wa mwaka 2002 unampatia ruhusa Mwalimu Mkuu au Mwalimu atakayepewa ruhusa kwa maandishi kutoa adhabu kwa mwanafunzi viboko visivyozidi vinne kwa wakati mmoja na kosa ambalo ataadhibiwa ni kosa la jinai au nidhamu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo liliotokea Mei 14 mwaka huu majira ya saa nne asubuhi wakati mtihani wa moko ukiendelea katika shule hiyo, na alipigwa viboko sehemu mbalimbali za mwili wake ila aliumiza zaidi mgongoni.
Alisema, upepelezi wa tukio hilo unaendelea na utakapokamilika Mwalimu huyo atafikishwa mbele ya mahakama kujibu tuhuma zinazomkabili lakini uchugunzi wa awali unaonesha mwanafunzi huyo aliadhibiwa kwa kufutafuta jina lake kwenye karatasi ya majibu wakati wa mtihani huo.
Awali akisimulia tukio hilo, mama mzazi wa mwanafunzi huyo Pauline Benedicto alisema, ilikuwa majira ya asubuhi ya tarehe 14 aliamka mapema kumuandalia mwanae chakula kwa sababu alikuwa kwenye mitihani na alipokuwa njiani kumpelekea alikuwa nae huku akiwa analia kwa uchungu.
Alisema, wakati akimhoji kulikoni kwanini analia ghafla alianguka chini na kumbeba mpaka nyumbani na kumhadithia kuwa ameshambuliwa kwa viboko na Mwalimu mkuu wake, ndipo alipochukua jukumu la kutoa taarifa katika uongozi wa serikali ya kijiji na mtendaji wa kata.
Pauline alisema, kutokana na maumivu aliyokuwa akiyasikia mtoto wake waliandikiwa barua ya kumpeleka zahanati kupata huduma ya kwanza wakati wakimsubiria Mwalimu Mkuu kufika ofisi za kata kwa ajili ya kuyazungumza, lakini alishindwa kufika kwasababu alikuwa miongoni mwa wasimamizi wa mitihani.
Aidha alisema, walifika shuleni na Mwalimu mkuu alikili kumpiga viboko mtoto wake kwa sababu ya kukosea mara kadhaa kwenye karatasi ya majibu wakati akifanya mtihani wa moko, na kutokana na hasira alizokuwa nazo alimpiga kupitiliza na kuomba msahamani juu ya tukio hilo.
Nae mwanafunzi huyo alisema, alikosea kuandika jina lake kwenye karatasi ya majibu wakati wakifanya mtihani wa moko ikachafuka, Mwalimu mkuu alimsimamisha mbele ya wanafunzi akimtaka kuandika ubaoni jina lake huku akimshambulia kwa viboko sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ngilimba, Zuberi Mabula alisema,hatua waliyoichukua baada ya kupokea malalamiko hayo walimshauri Mwalimu mkuu kukaa na familia ya mtoto huyo na kumtibisha, lakini hakuweza kutekeleza hayo hali iliyowafanya kutoa taarifa kituo cha polisi kwa hatua zaidi za kisheria.
Katibu wa CCM wilaya ya Kahama Andrew Chatwanga alisema, mtoto huyo ameumizwa sana na kitendo alichofanya Mwalimu mkuu sio cha kiungwana na hakipaswi kuvumilika kwenye jamii, kwani anamajeraha ya viboko mpaka kichwani hali ambayo ni hatari sana.
Mbunge wa jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani akiwa kwenye mkutano wa hadhara kijijini hapa aliahidi kumsaidia mtoto huyo kupata matibabu ili apone na kuendelea na masomo kwani darasa alilopo ni la mitihani, na kuliomba jeshi la polisi kukamilisha upelelezi na kuchukua hatua.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED