Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamekosoa vikali uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, wa kutengua uongozi uliochaguliwa na vikao halali vya chama kufuatia barua ya mwanachama Lembrus Mchome.
Akizungumza kwa niaba ya chama, Wakili Dickson Matata alisema Msajili hana mamlaka ya kutengua viongozi wa chama chao na kwamba utenguzi huo una malengo ya kisiasa badala ya malengo ya kujenga chama hicho.
“Kisheria, Msajili hana mamlaka ya kutengua uongozi wa chama uliochaguliwa kwa mujibu wa Katiba ya chama. Hii si mara ya kwanza, alishawahi kufanya hivyo kwa NCCR-Mageuzi,” alisema Matata.
Walisema kuwa barua hiyo haikuambatanisha ushahidi wowote na hatua ya Mchome ya kwenda kwa Msajili badala ya Mahakama, ni ishara ya nia ovu yenye malengo ya kisiasa.
CHADEMA imetoa wito kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria kwa kulea vyama badala ya kuvigombanisha au kuviua. Pia imewataka wanachama wake kupuuza barua kutoka kwa Msajili, wakisema haina msingi wa kisheria.
Mwisho wa taarifa hiyo, viongozi wa chama wamesisitiza kuwa bila marekebisho ya mfumo wa uchaguzi, CHADEMA haitashiriki uchaguzi wowote, wakirejea kauli yao: “No Reform, No Election.”
Kimesisitiza msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi wowote hadi mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi yatakapofanyika, kikieleza kuwa kauli ya "No Reform, No Election" ni maamuzi halali ya vikao vya juu vya chama na si ya mtu binafsi.
Viongozi hao walisisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi haina uhalali wa kusimamia uchaguzi huru kwa sababu ya kuwa na uhusiano wa karibu na chama tawala, CCM. Aidha, walihoji uhalali wa wakurugenzi wengi wa tume hiyo wanaotoka CCM, pamoja na mgawanyo wa majimbo unaodaiwa kufanywa kwa upendeleo.
“Ni wazi kuwa mfumo wa sasa hauwezi kutoa uchaguzi wa haki. Mabadiliko ya sheria na mfumo wa tume ni ya lazima kabla ya kushiriki uchaguzi mwingine wowote,” aliongeza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED